Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

CHRISTMAS I, DECEMBER 25, 2006
A SERMON BY PETER K. MSENGI BASED ON Mathew 2:13 – 23
(->current sermons )


YESU KRISTO MWANA WA MUNGU

“ Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu
alimtuma mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke,
amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao
waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea
hali ya kuwa wana”. Gal. 4: 4 – 5
Ujumbe wa leo unapatikana kutoka Injili ya Mathayo 2:13 – 23

Utangulizi

Kulingana na somo hili tunaona muendelezo wa historia ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo mwana wa Mungu. Baada ya kuzaliwa kule Bethlehemu, wakati ule Mashariki ya mbali kulitokea nyota iliyowaongoza Mamajusi (wataalamu wa nyota). Watu hawa walipoangalia vitabu vyao waligundua kuwa mfalme alikuwa amezaliwa kule Uyahudi katika mji wa Daudi. Kipindi hiki utawala wa nchi ya Israeli ambao uligawanyika katika sehemu kuu mbili Kusini na Kaskazini, ulikuwa koloni la milki ya dola ya Kirumi. Hivyo kiongozi aliyetawala ni Herode upande wa Juda na Samaria, mwanawe Akelaus alishika eneo la Idumea pamoja na endol la babaye alipokufa 6AD. Wataalamu hasa walifika Yerusalemu wakakutana na Herode wakamwuliza habari ya kuzaliwa kwa mfalme huyu Yesu Kristo. Jambo hili lilimshtua sana Herode na hata kughadhabika. Akawasihi wale Mamajusi ya kwamba waende hadi Bethlehemu wakapeleleze na wakaiisha kumwona warudi kwa njia ile ile ili wamletee habari kamilifu mfalme Herode naye aende kumsujudia. Mungu alikuwa ameona moyo wa Herode ulivyowaka ndani yake na ndipo sasa tunaendelea kuona jinsi Mungu alivyomlinda mwanawe.

Kukimbilia Misri (Ulinzi wa Mungu)

Wapendwa wasomaji Biblia katika Mathayo 2:13 inatuambia kuwa Mungu alimtokea Yusufu mlezi kwa njia ya ndoto akimwambia, “Ondoka, umchukue mtoto na mama yake ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Ndugu wapendwa tendo hili ndilo linaloonyesha hali ya tabia ya wivu wa mwanadamu wa kutotaka kuwa mdogo katika mamlaka ya Mungu. Herode amepata mashaka juu ya nafasi ya uongozi wake yaani amefikiri juu ya kukosa cheo. Lakini Mungu anaweka njia tofauti na mawazo ya Herode.

Mungu amewaonya Mamajusi wasipeleke habari kwake Yusufu ametoroka usiku na mtoto pamoja na mama kwenda Misri. Pengine tendo la Yusufu kumkimbiza Yesu Misri linakumbusha Historia ya Ukombozi wa taifa la Israeli lililotokea huko Misri. Pia tunamlinganisha Yesu kama vile Musa alivyofanyiwa na Farao (Kut. 2: 1 – 15). Lakini Biblia inatuambia kuwa kutendeka hayo ilikuwa ni ukamilifu wa andiko lililotabiriwa na Nabii Hosea ya kwamba taifa la Israeli liliitwa mwana likiwa Misri na huko alilitoa utumwani. Taifa jipya ambalo Mungu amelitengeneza ni Kanisa lake kwa njia ya Yesu Kristo. Watu walioishi katika utumwa wa dhambi ambao ni mimi na wewe.

Jambo la Pili Kuuawa kwa Watoto

Baada ya Herode kugundua kuwa wamemdanganya basi alipitisha uamuzi wa kuangamiza watoto wote wa kiume walio na umri wa miaka miwili na kwenda chini kulingana na maelezo ya wale Mamajusi. Kweli kitendo hiki ni kibaya sana chenye kuonyesha ukatili wa hali ya juu. Hofu ya kukosa ufalme ilimlazimu Herode afanye kosa kubwa la mauaji haya mabaya ya damu isiyo na hatia. Wapendwa leo hii tunasikia viongozi wengi au watawala wengi wakiwaua watu wanaowadhania wanataka kuwapindua, mifano ni mingi sana mf. Somalia, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Iraq, Iran, Marekani nk. Watawala hawa wametumia mabavu katika kutawala wengine na mauaji makubwa yamefanyika. Haya yamefanywa kwa tamaa ya madaraka, wivu, chuki na hata ukabila au uchumi.

Roho ya uongozi wa aina hii unalinganishwa na hali iliyotokea kule Rumi, kilio na maombolezo mengi Raheli aliyowalilia watoto wake asikubali kufarijiwa. (Yer. 31:15). Mji wa Rumi ulikuwa maili nane (8) kusini ya Yerusalemu mji mkuu ulitekwa na kupelekwa utumwani Babeli, hivyo vilio vilisikika kwa wakati wa vita vile. Huu ni mfano wa machungu ya wanawake waliowalilia watoto wao waliouawa kikatili na Herode. Lakini Bwana aliwafariji akisema zuia sauti yako, usilie na macho yako yasitoe machozi, … tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema Bwana, na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe. Kwa maneno ya uchungu, Mungu anajenga matumaini ya akina mama kuwa watafurahi. Hii ndiyo hofu na mashaka iliyowakumba wazazi wa Yesu, lakini Mungu anasema nao wakiwa ugenini Misri ya kuwa warudi tena nyumbani Yuda.

Wakati wanarudi habari zilisikika kuwa mtoto wa Herode anatawala, Mungu akawaonya wasirudi Bethelehemu bali wapande kwenda Nazareti ili andiko litimilike kuwa ataitwa Mnazarayo. Kitendo hiki kilipelekea kuonyesha jinsi Mungu alivyojishughulisha na ulinzi wa mwanawe.

Ujumbe

Wapendwa wasomaji ni vyema tutambue kwamba Mungu ni mkuu kuliko tunavyodhani. Somo hili linakusudia kumdhihirisha Yesu kuwa alikuwa mwana wa Mungu kweli kweli aliyempa ulinzi wa kutosha ili kusudi lake la kutukomboa litimie. Paulo katika Warumi 8:16 – 17 anatueleza kuwa Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu tuliofundishwa pamoja naye toka utumwa wetu wa dhambi yaani tunahesabika kuwa warithi pamoja naye. Kwa sababu Mungu alimtuma mwanawe atukomboe sisi tulio chini ya sheria.

Hebu jiulize swali hili kati ya Mamajusi na Herode wanakupa funzo gani? Mamajusi wanaleta funzo la utii juu ya maonyo ya Bwana. Je ni mara ngapi wewe umeonywa na Roho Mtakatifu kutotenda uovu? Je umemsikiliza Roho akushaurivyo au umezidi kuwa na shingo ngumu na kuendelea kumsaliti Yesu kwa ibilisi. Herode anatumika nafasi ya shetani, roho katili isiyotubu wala kukubali kupokea wokovu wa Bwana na anaangalia mambo yake binafsi tu.

Wapendwa Yesu aliyezaliwa na kupita hatua zote za Historia ya Ukombozi wa Israeli alikamilisha hatua zote za Agano la Kale na hivyo kulitimiliza Agano Jipya kwa taifa teule jipya linalokombolewa kwa damu yake. Mathayo anauona ukamilifu siyo katika Historia ya Israeli tu, bali katika tukio la kuzaliwa Kristo ni mfano wa wakristo wanapozaliwa katika maisha mapya inapowapasa kutafutwa na maadui ili kuwaangamiza, wasiofu kwani Mungu ndiye atakayewapigania na kuwapa ulinzi wa kutosha hata uzima wa milele. Kumpokea Yesu ni saa na kuwasha kurunzi safarini mwako wakati wa usiku wa giza. Yesu atakuongoza na kukukamilisha hata uzima wa milele.

Tuombe : Mungu tunakushukuru kwa ulinzi wako kwetu sisi uliotuzaa upya kwa njia ya kumpokea Yesu Kristo, uliyemleta hapa duniani kwa njia ya kuzaliwa na Bikira Mariamu na kumpa ulinzi wote. Hivyo utuimarishe mioyoni mwetu tuondoe hofu na mashaka dhidi ya maadui watuzungukao maishani mwetu. Utufikishe katika ukamilifu wa uzima wa milele, kwa Yesu Kristo. Amen.

Mch. Peter K. Msengi,
Chuo cha Theologia Mwika,
S.L.P. 3050,
MOSHI – TANZANIA.
E-mail: mwika@elct.org

 


(top)