Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

Christmas Eve 24.12. 2006
A Sermon Based on Isaiah 9: 2-7 (UV) by Awumsuri Masuki
(->current sermons )


“Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru kuu imewaangaza. Umeliongeza taifa, Umezidisha furaha yao, wanafurahi mbele zako, kama furaha ya wakati wa mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake na gongo la bega lake na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyoviringishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake, mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe, katika kiti cha enzi cha daudi na ufalme wake, kuuthibitisha na kuutegemeza kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele. Wivu wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”Amen.

Utangulizi

Kitabu cha Nabii Isaya milango ya 6-12 kinaitwa kitabu cha Imanueli kwa sababu habari nzima ya kuja kwa Mesiya kuuokoa ulimwengu imetabiriwa katika kitabu hiki. Utabiri wa Nabii Isaya ulionyesha jinsi Mungu alivyoamua kuwa pamoja na Yuda ili kuwapa ukombozi mkubwa dhidi ya maadui wake Syria (Resini) na Israeli (Peka). (Isa. 7-9). Jina Imanueli yaani Mungu pamoja na wanadamu, limetajwa akimaanisha mkombozi wa taifa la Israeli kutoka katika mateka na uhamisho wa Babeli ambapo Mwajemi Kureshi alitimiza mwaka 539 K.K.

Jina hili ‘Imanueli’ linatajwa tena na malaika alipompa Mariamu habari za kumzaa mkombozi wa dunia yote atakayewaokoa watu kutoka utumwa wa dhambi, akisema “Tazama bikira atachukua mimba naye atamzaa mwana, nao watamwita jina lake Imanueli; yaani Mungu pamoja nasi” (Mathayo 1:23)

Siku hii ya leo tunakumbuka tukio lile ambalo lilitikisa nguvu za mbinguni na za duniani zikishangilia na kutangaza ukombozi ulioujia ulimwengu wote. Siku hiyo, Malaika Mbinguni walishangaa kuona Mungu akija kukaa na wanadamu, nao wakashuka kuja kumhudumia. Hawa ndio waliotangaza habari kwa wachungaji wakiwa makondeni kuchunga mifugo yao(Luka 2:14). Tena tukio hili linawagusa wataalamu wa dunia hii kuacha shughuli zao na kuongozana kwenda kumsujudia Yesu Kristo mwokozi wa watu wote(Mathayo 2:1-2). Hata ufalme uliokuwepo ulitikisika na Mfalme Herode na Yerusalemu yote walifadhaika na kuwa na kikao kumjadili.(Mathayo 2:3f.)

Kwa ulimwengu wote ni tukio la furaha sana kwani yeye aliyezaliwa leo ni mkombozi atakayewaokoa watu wote na uovu wao.

YESU KRISTO AMEZALIWA- HALELUYA

(Ni Mungu Katikati Ya Wanadamu)

Kuzaliwa kwa Yesu Kristo duniani ni nguvu ya Mungu imetufikia. Yeye ndiye aliyengojewa tangu zamani na baba zetu kwa ukombozi walioelezwa kuwa utawajilia tangu anguko la Adamu. Kuzaliwa kwa Yesu kunathibitisha utimilifu wa unabii na kila kiumbe kitauona wokovu wa Mungu wetu. Mambo kadhaa yametimia kufuatia kuzaliwa kwa Yesu.

1. Giza limeondoshwa na nuru imetawala

Yesu Kristo anaondoa giza lililowazuia watu wasimwone Mungu. Watu wanakombolewa kutoka dhambi na uasi unaowafanya watu wasimtii Mungu. Yesu amezaliwa ili awafanye wote wamtii Mungu. Yohana katika waraka wake anashuhudia habari za Yesu na nuru yake ulimwenguni akisema “Kulikuwako nuru halisi amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu” (Yohana 1:9)

2. Mauti imeondoshwa na uzima unatawala

Yesu anaondoa kivuli cha mauti. Watu wote walihukumiwa kufa tangu lilipotokea anguko la adamu. Yesu alikuja kutangaza uzima tutakaoupata hapa duniani, na baada ya maisha haya. Amekuja kuwahubiri maskini habari njema, kuwafungua waliofungwa, kuwafumbua vipofu macho, kuwaweka huru walioteswa na kuwatangazia watu mwaka wa Bwana uliokubalika.(Luka 4:18) Kuzaliwa kwa Yesu ni ushindi dhidi ya mauti ya milele. Yesu anasema: “Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” (Yn 5:24)

Kuzaliwa kwa Yesu ni furaha kubwa maana amefungua nira za uovu na kumfungia kila anayemwamini nira za uzima. Amezima mishale ya maadui na kuweka uhuru kwa ulimwengu wote. Kwa hiyo, Yesu ameleta utawala mpya. Ameweka agano jipya kuwa Mungu sasa amefanya maskani yake pamoja na wanadamu wote. Anataka ulimwengu wote-mimi na wetu tumgeukie na kumtii na kumtegemea yeye siku zote.

3.Yesu Kristo ni Kiongozi Shujaa Aletaye Utawala wa Amani

Tumepewa mtoto mwanamume. Huyu ni zawadi ya ajabu toka kwa Mungu na ni uzima wa watu. Mtoto huyu ana vipawa bora vyote walivyohitaji mashujaa wote wanaotawala duniani. Dunia imepata mtawala aliye bora zaidi. Katika waraka kwa Waebrania tunasoma kuwa Yesu amefanyika kuwa bora kuliko Malaika na tena kuliko Musa na manabii. Amejawa na hekima mfano wa Mfalme Sulemani-huyo atawaamua watu wa Mungu kwa haki. Anao uwezo wa kiMungu katika utendaji wake; ni Baba asiyekoma (wa milele) hata wanadamu wakiwa wakorofi, atawatawala kwa amani.

Huyu ndiye atakayeupatanisha ulimwengu wenye dhambi na Mungu aliye mtakatifu yaani atawafanya wote wamwamini Mungu kama baba nao ni wana.

Ataleta amani kati ya mtu na jirani yake, taifa na taifa lingine, kabila na kabila lingine, dini na dini nyingine, weusi na weupe, matajiri na maskini, Wayahudi na wasio wayahudi, na watu wote(wadhambi) na Mungu aliye Mtakatifu. Yesu Amejawa na Roho ya kumcha Mungu, naye ataamsha dhamira ya kumcha Mungu na kumwabudu. Watu wote watamwogopa Mungu, naye Mungu mwenyewe atawachunga watu wote kwa upole. Kutakuwa na Mchungaji mmoja na kundi moja Hii ni neema ya Mungu wetu

Kuzaliwa kwake Yesu ni mpango wa Mungu wa kuondoa uadui ambao umetawala duniani. Nabii Isaya akitabiri habari za wokovu mkubwa utakaotokea kwa kuja kwa mesiya duniani anasema “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi, ndama na mwana-simba na kimono watakuwa pamoja na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu…” (Isa. 11:6-9). Kwa kweli huu ni ukombozi mkubwa kwa kila kiumbe.

Mpendwa mtu wa Mungu, Yesu Kristo amezaliwa na ni mwokozi wa ulimwengu mzima. Habari hii iliyotokea takribani miaka elfu mbili na saba iliyopita, nguvu yake inafanya kazi hadi leo na itaendelea vizazi vyote pasipo mwisho. Inatupasa kujua kwamba;

  • Yesu analeta amani ndani ya kila mtu anayemwamini na kumpokea, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” (Yn. 1:12)
  • Anafanya maisha ya jamii yawe ya haki na ya amani. Anasitisha ugomvi kati ya mtu na mtu, taifa na taifa,n.k
  • Anaweka amani kati ya mwanadamu na viumbe wengine. Anastawisha mifugo na mimea kwa ajili watu. Yesu Kristo anaweka uhusiano bora kila upande.

Tufungue mioyo yetu sasa, tumkaribishe Yesu azaliwe ndani yetu ili alete mabadiliko ya kweli, na ulimwengu mzima kwa njia ya mtu mmoja mmoja, ukombolewe na kupata amani ya kweli.

Bwana na atujalie sote kumpokea mwokozi wetu kwa furaha.

“YESU KRISTO AMEZALIWA- HALELUYA” Amen.

Rev. Awumsuri Masuki
Mwika Bible School
P.O. Box 3050
Moshi.
E-Mail: ajmasuki@yahoo.com

 

 


(top)