Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

FOURTH ADVENT, DECEMBER 24, 2006
A SERMON BY REV. OBED M. AKYOO BASED ON LUKE 1:39 – 44
(->current sermons )


1. Utangulizi

Mpendwa msomaji upo usemi unaosema “Mwanadamu si Kisiwa”. Usemi huu unaonesha jinsi ambavyo binadamu tunahitajiana, tena mwanadamu hawezi kujikamilisha peke yake, lazima kuhusiana kwa sababu mbalimbali mfano kubadilishana uzoefu, kufarijiana na hata kusaidiana kwa sababu mtu ni watu.

 

Mpendwa msomaji katika somo la leo, tunamuona Mariamu na Elisabeti wakidhihirisha ukweli wa usemi nilioutaja hapo juu. Mariamu anachukua hatua ya kufanya ziara ya kumtembelea mwenzake Elisabeti. Katika ziara hii tunaona wakibadilishana uzoefu na kufurahia baraka na neema walizopewa na Mungu.

2. Tuwe naUshirika Wa-aminio

Mpendwa msomaji Neno la Mungu linatuhimiza “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine…” (Ebr. 10:25) Mariamu na Elisabeti ambao Mungu aliwatendea muujiza inayofanana wanakutana katika ushirika wa-aminio. Haina maana Mariamu alikuwa na mashaka juu ya ujumbe wa malaika Gabriel (Lk. 1:30) hata kuhitaji kuthibitisha aliyojulishwa juu ya Elisabeti (Lk. 1:36). Mariamu wala hakujali kule kubeba mimba jamii ya wakati ule ingemfikiria nini kwani lilikuwa si jambo la kawaida binti kubeba mimba katika jamii ya wakati huo. Lakini Mariamu hakujali hayo bali alimtii Mungu. Aidha Mariamu alichohitaji ni ufafanuzi jinsi utaratibu wa Mungu utakavyokuwa (Lk. 1:34). Lakini Mariamu anaamini aliyoambiwa, ndiyo maana anasema “ Tazama mimini mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema (Lk. 1:38). Lengo la Mariamu katika ziara hii lilikua ni kutafuta kuwa na ushirika na mwenzake Elisabeti na sio vinginevyo.

Mpendwa msomaji sawa sawa na ahadi ya Neno la Mungu walipo wawili au watatu naye Mungu yupo mahali hapo. Hapa katika ushirika huu tunaona uwepo wa Mungu kati ya hawa kinamama wawili. Katika hali isiyotegemewa Roho Mtakatifu anamjaza Elisabeti. Roho Mtakatifu anamwezesha Elisabeti kumtambua Bwana wake (Yesu Kristo) hata kabla ya kuzaliwa na kutambua kuwa Mariamu amebeba mimba ya Masihi. Mpendwa msomaji katika ushirika huu tunajazwa Roho Mtakatifu ambaye ni faraja yetu, mwalimu anayejulisha mapenzi ya Mungu kwetu.

2.1. Ushirika wa-aminiounaleta furaha ya pekee kwa washirika

Mpendwa msomaji, baada ya Mariamu na Elisabeti kusalimiana wanajawa na furaha ya pekee. Aidha zaidi ya wao kufurahi, tunaona hata watoto waliopo tumboni wanasalimiana kwa ishara ya kurukaruka tumboni.

Mpendwa msomaji, Ushirika wa-aminio unaondoa huzuni zetu na kuzigeuza kuwa furaha na faraja kubwa. Baadhi kwa kutokuwa na Ushirika kama huu wa kiroho, wamefikia hatua ya kukata tamaa, kujawa na huzuni, upweke na hata baadhi wamefikia hatua ya kujiondoa duniani, baada ya kuona hawana sababu ya kuendelea kuishi. Zipo sababu nyingi za sisi kudumisha ushirika wa-waamino kwani tunahitaji kusikia shuhuda za wenzetu wanavyotendewa na Mungu, tena tunahitaji kuimarishana kiroho, tunahitaji tufanye kama mitume wa kwanza ambao siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakiumega mkate nyumba kwa nyumba na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe (Mdo. 2:46).

Mpendwa msomaji, wapo baadhi ambao wamechoka kukutana na wenzao katika ushirika wa waaminio. Wao wanadai kuwa hakuna haja ya kuwa na Ibada na wenzao kwa sababu wanatazama Ibada kwenye Televisheni. Tukumbuke usemi unaosema ukuni unaowaka ukikaa peke yake ni rahisi kuzimika, hii ina maana Mkristo akiendelea kujitenga na wenzake katika Ibada itafikia hatua atapoa kabisa ki-imani hata kufa kiroho. Tukumbuke kuwa na ushirika na wenzetu ni zaidi ya mikutano ya kawaida ya kijamii, Katika ushirika huu Mungu yu kati yetu. Mpendwa msomaji, fanya uamuzi Noel ya mwaka huu anza kujumuika na wenzako katika Ibada, soma Biblia, mikutano ya Injili nk. Utaona baraka za Mungu.

2.2. Ushirikawa-aminio ni faida si tu kwa watu wazima lakini hata kwa watoto wetu.

Mpendwa msomaji, mbali ya wazazi hawa wawili kufurahi na kuimarishana kiroho hata watoto waliopo tumboni tunaona wakiruka tumboni kama ishara ya furaha. Watoto wanaozaliwa katika familia za wakristo wanaomcha Bwana ni hakika nao pia watakua katika hali hiyo hiyo ya kumpenda Mungu. Neno linasema “Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha, hata akapokuwa mzee (Mith. 22:6). Wazazi wa mtoto Yohana, yaani Elisabeti na Zakaria na wazazi wa mtoto Yesu Mariamu na Yusufu wanatajwa kuwa wazazi waliompenda Mungu na kuziamini ahadi zake Mungu. Aidha tunaona watoto wao wanakua katika kumpenda na kumtii Mungu. Mpendwa msomaji, unawakuza watoto wako katika misingi ipi? Je umepata nafasi ya kukaa na watoto kusoma neno la Mungu na hata kuomba pamoja? Malezi ya mtoto yanapaswa kuanzia tangu mtoto akiwa tumboni, usisubiri hadi siku ya kuzaliwa utakuwa umechelewa. Tazama hawa wazazi wanawabariki watoto wao tumboni, kumbuka Mungu aliyewapa ujauzito na kuwaombea watoto. Mpendwa msomaji, Je umepata nafasi ya kuwaombea watoto ambao bado hawajazaliwa na kuwabariki?

Baadhi ya watoto wameathirika tangu tumboni. Baadhi ya wazazi wanawachukia watoto wao tangu tumboni, wapo ambao wanajaribu kuwatoa watoto tumboni, wapo ambao hawafurahi kuwa Mungu amewapa baraka ya ujauzito na watoto hawa wanapozaliwa wanazaliwa katika familia ambazo hawapo tayari kuwapokea, familia zilizojawa na chuki, hakuna amani, matokeo yake watoto hawaoni upendo wa Mungu na kufanya maamuzi ya kukimbia nyumbani. Mpendwa msomaji hali hii imezidisha watoto wa mitaani na kuzidisha vikosi vya majambazi katika jamii. Mpendwa msomaji, ebu katika Noeli ya mwaka huu tafuta uhusiano na watoto wako na uwavute watoto kwa upendo wampokee Kristo anayezaliwa ndani ya maisha yao afanye mabadiliko katika maisha yao.

3. Ushirikawa-aminio unaondoa tofauti zinazotutenganisha wanadamu

Mpendwa msomaji, ni ukweli usiopingika kuwa hawa akina mama walitofautiana katika mengi, kwa mfano tofauti za ki-umri ingeweza kuwa sababu tosha ya kushindwa kukaa pamoja hawa ki-namama. Elisabeti amepata ujauzito katika umri wa uzee wake wakati Mariamu anapata ujauzito katika umri wa usichana wake akiwa bikira. Pamoja na tofauti hizi tunaona hawa kinamama wanakutana kwa furaha tena Elisabeti anampa heshima kubwa Mariamu yeye na mtoto wake – Elisabeti anasema, “ Limenitokaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” (Lk. 1:43). Mpendwa msomaji, katika hali ya kawaida iliyotawaliwa na mila na desturi zetu isingewezekana kutokea hali hii. Lakini katika ushirika wa-aminio jambo hili linawezekana kwa sababu Roho Mtakatifu ndiye anayetawala. Katika dunia ya sasa, tunashuhudia ufa unaozidi kujengeka kati ya mataifa yaliyoendelea na mataifa ya ulimwengu wa tatu. Aidha ufa kati ya nchi maskini na nchi tajiri unaongezeka siku hadi siku. Watu maskini wanazidi kuwa maskini na walio tajiri wanazidi kuwa matajiri. Je hili ndilo kusudi la Mungu kutupa vipawa na rasilimali mbalimbali? Mpendwa msomaji, ni dhahiri kuwa tungetafakari rasilimali na vipawa tulivyopewa na Mungu katika mtazamo na mapenzi ya Mungu hali iliyopo ya chuki, ubinafsi duniani isingeendelea kuwepo. Tungerudi katika ushirika ambao tutashirikiana vipawa na mali zetu katika hali ya usawa.

4. Hitimisho

Mpendwa msomaji, umefika wakati wa kumrudia Mungu. Katika Noeli ya Mwaka huu ni nafasi aliyotupa Mungu kwa neema yake tutubu pale ambapo tumejitawala sisi wenyewe. Tuige mfano wa Mariamu na Elisabeti kuunda ushirika wa-aminio. Zoezi hili lianzie katika familia zetu tuwe na nafasi ya kusifu, kusoma Neno, kuomba kati yetu wazazi na watoto. Aidha tusiache kujumuika na wenzetu katika Ibada, masomo ya Biblia, mikutano ya Injili nk. Mpendwa msomaji, pasipo kujali jamii inasema nini, uwe tayari Kristo azaliwe moyoni mwako katika Noeli hii, anasema, Tazamanasimama mlangoni, nabisha, mtu akisikia sauti yangu na kuufungua mlangonitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami (Uf. 3:20). Yesu Kristo yupo tayari kuzibeba huzuni zako na kukupa amani tena ataleta fruraha ndani yako, familia yako na mwisho atakupa uzima wa milele. (Yoh. 11: 25 – 26) Amen.

Rev. Obed M. Akyoo,
P.O. Box 3050 ,
MOSHI – TANZANIA.
E-mail: mwika@elct.org

 

 

 


(top)