Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

III ADVENT 17, DECEMBER, 2006
A SERMON BY AMINI A. NJAU BASED ON LUKE 3:1-6
MTANGULIZI WA YESU KRISTO (YOHANA MBATIZAJI)
(->current sermons )


Sura ya 3 na sura ya 4:1-13, ni maelzo juu ya maandalizi ya kazi ya Yesu Kristo ya kufundisha Injili. Aidha inatueleza juu ya Yesu Kristo kufikia utu-uzima na sasa mwandishi anatuonyesha jinsi Mungu mwenyewe alivyoandaa mpango mzuri, na matayarisho mazuri na hata mazingira mazuri kwa Yesu kuanza kazi aliyoijia duniani. (Yoh. 3:16; Iyohana 4:9).

Yohana Mbatizaji aliandaliwa na Mungu na alikuwa mjumbe wa Mungu aliyetumwa kumwandalia Yesu njia. (Marko 1:2-5). Nabii Isaya naye alitabiri juu ya kuja kwa Yohana Mbatizaji. “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa na kila mlima na kilima kitashushwa …” (Isaya 40:3-5; Mathayo 3:3-).

Yohana Mbatizaji, mtoto wa Zakaria na Elizabeth, dadaye Maria Mama yake Yesu, alizaliwa katika mazingira ya pekee kuonyesha bayana kwamba Mungu alimwandaa kwa kazi maalum. (Kumwandalia Yesu njia). Wakati huo walikuwepo wale watawala wa Kiyahudi ambao hawakumpenda Yesu, hasa Herode, akiwa mfalme wa Galilaya. Pontio Pilato alikwa Liwali wa Uyahudi, Filipo nduguye Herode alikuwa mfalme wa Iturea na Trakonti, na Lisania alikuwa mfalme wa Abilene. Tiberio alikuwa ndiye Kaisari. Katika kipindi hicho Kuhani mkuu alikuwa Anasi na Kayafa. Huu ulikuwa wakati mgumu kuzungumza habari za Injili ukizingatia utawala uliokuwapo madarakani haukutaka kusikia habari za Yesu.

Ni katika wakati wa watawala hao, mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, neno la Mungu lilimfikia Yohana mwana wa Zakaria wakati akiishi jangwani. Alipita jangwani, nchi ya Yordani na bonde la Yordani. Yohana alihubiri na kufundisha juu ya ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi. Mahubiri yake yalishatabiriwa na nabii Isaya. (Isaya 40:3ff).

MAHUBIRI YA YOHANA MBATIZAJI

Mwandishi Luka anaonyesha wazi wakati wa mahubiri ya Yohana na mwanzo wa mahubiri ya Yesu Kristo – Tunaweza kuona kuwa ni kati ya B.K. 28-29, Tiberio alipokuwa mtawala. Yohana alihubiri ubatizo wa toba kwa ondoleo la dhambi. (Marko 1:4). Neno ambalo Yesu mwenyewe alilipa mkazo mkubwa baada ya kufufuka kwake. (Luka 24:4-7).

UJUMBE WA YOHANA UNATUGUSA SISI LEO

Bwana Yesu anataka kuingia katika mioyo yetu, lakini ni lazima tumwandalie njia aweze kuingia.

Mioyoni mwetu mna mabonde, milima na vilima, visiki, kuparuza n.k. kwa maana kwamba katika mioyo yetu kuna mambo kadhaa yasiyompendeza Mungu, hayo hatuna budi kuyaondoa Yesu apate kuingia. Yaliyoko katika mioyo yetu kwa kweli hayampendezi Mungu: Chuki, hasira, fitina, uadui, ubinafsi, tabia ya zinaa, i.e. uasherati, maonevu na ufisadi wa aina mbalimbali.

Wako wanaofikiri labda wakifanya maasi kwa siri wako salama na mara nyingi hawatubu na kutengeneza njia zao. Bila toba, tutaangamia. (Yoh. 3:36). Chukua mfano wa mtu anayepokea rushwa na kumudu kujenga nyumba yake nzuri na kuishi kwa furaha na familia yake. Asipotubu kosa hilo, Yesu hawezi kuingia kwake kwa sababu mlango wa moyo wake umefungwa, aidha njia ya moyoni kwake ina mabonde, milima, visiki, miiba n.k. Haya ndiyo Yohana Mbatizaji anasema tuyaondoe, tumtengenezee Bwana njia nyofu, hatimaye tuweze kuurithi uzima wa milele.

Mkosaji asipotubu dhambi yake, basi hutembea nayo kila siku, kila mahali, na siku moja itamuumbua. Angalia sana dhambi yako isikuumbue hadharani na kukukosesha ufalme wa mbinguni.

Mfano:
Siku moja mgeni alifika kwenye nyumba ya mama mmoja aliyeitwa Janeth. Ilikuwa saa 5.00 hivi, mgeni aliyevalia vizuri, juu kavaa koti kubwa, akaonekana mtanashati kweli kweli.

Mama alimkaribisha apumzike sebuleni wakati yeye akiandaa chai na chakula cha mchana ili awahi kumtunza mgeni wake ambaye alijitambulisha kuwa rafiki wa karibu wa mume wake.

Baada ya shughuli kuendelea, mama (Janeth) alikwenda sebuleni kuangalia saa ili mtoto wake mdogo ajiandae kwenda shule. Aliangalia kila pembe pale sebuleni hakuona saa, akasema kwa sauti ya chini na mgeni alimsikia, “Ha! Saa ya mezani imekwenda wapi?” naye mgeni akasema, “Nilipoingia hapa sikuona saa hapa mezani.” Janeth alitafuta kila mahali bila mafanikio.

Chakula cha mchana kiliiva mapema ili mtoto wake ale aende shule na pia awahi kumtunza mgeni rafiki wa mume wake aliyekuwa amejitambulisha kwa jina moja, “Magesho”.

Wakiendelea kula yapata saa sita kasoro dakika tano hivi, mama alizidi kuguna na kusikitika juu ya saa yake ya mezani. Watoto wawili wa mama walikuwa nao wanakula mezani, nao wakisikitika juu ya kutoweka kwa saa yao ambayo waliitegemea sana kuangalia saa za kwenda shule.

Mgeni – Magesho aliendelea kula bila wasiwasi. Ilipotimia saa sita kamili ile saa iligonga kengele kwa sauti kubwa mfukoni mwa koti kubwa la yule mgeni. Alipatwa na wasiwasi na mahangaiko. Mama na watoto walipiga kelele za shangwe, “Hiyo ile saa, mgeni anayo mfukoni” Mama alipiga yowe kwa nguvu kuomba msaada wa majirani kwani aligundua kwamba yule mgeni alikuwa mwizi.

Majirani walifika wakamkamata na kumfikisha kituo cha Polisi.
NB: Dhambi zetu zitapiga kelele ndani yetu na kutuumbua hadharani.
Tutubu na kujiweka tayari kumpokea Yesu Kristo azaliwe katika mioyo yetu.

Pastor Amini A. Njau,
Evangelical Lutheran Church in Tanania,
Mwika Theological College of Tumaini University.
E-mail: mwika@elct.org
Personal E.mail: aminjau@yahoo.com

 

 


(top)