Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

MAHUBIRI KATIKA JUMAPILI YA I KATIKA MAJILIO (ADVENT I TAREHE 3/12/2006) YAMEANDALIWA NA MCH. ELISHIISA W. MBISE
MADA KUU: BWANA ANALIJIA KANISA LAKE.
NENO LA MAHUBIRI: YEREMIA 31:31 – 34
(->current sermons )


Nalo linasema hivi: Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya Agano Jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao asema Bwana. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana;Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu na jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena. Amen (The Holy Bible in Kiswahili Union Version)

UTANGULIZI

Mpendwa Msomaji wa mahubiri haya; Leo ni Jumapili ya kwanza ya majilio. Mada kuu inayotuongoza inasema; “BWANA ANALIJIA KANISA LAKE”. Kwa kawaida ukapokea ujumbe au taarifa kwamba kuna mgeni anayekuja kwako rasmi, au rafiki, au ndugu wa karibu siku au tarehe fulani maalumu; kwa mtu mkarimu lazima utajishughulisha sana katika kumpokea. Hivyo utatayarisha nyumba, mahali pa kulala, ratiba ya chakula itabadilika, ili kutafuta utakavyomridhisha ajisikie vizuri na kufurahi kufuatana na mazingira anayotoka. Na Waafrika wengi wana usemi usemao, “Mgeni ni Baraka” hivyo maandalizi ni muhimu.

Leo wakristo wote tumepokea ujumbe kwamba, Bwana analijia Kanisa lake. Kanisa ni wakristo, yaani mimi na wewe, ambao tunamwamini Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wetu. Je! Tumejiandaaje kumpokea kwetu wakati huu wa kuelekea kwenye sikukuu za Krismas?Je! ni mambo gani umeyaweka kipaumbele? Na Je! Ipo baraka gani katika kumpokea? Neno la Mungu tulilosoma; linatuweka tayari kumpokea na linatuonyesha baraka tutakazopata.

Nabii Yeremia ambae tumesoma sehemu ya Unabi wake kwa Taifa la Yuda, aliishi na kufanya kazi katika karne ya saba na sita kabla ya kuzaliwa Kristo. Wakati huo Taifa hili lilikuwa limevunja agano lao na Mungu kwa kutokutii, ambalo Mungu alilifanya na baba zao katika Mlima Sinai pale walipopewa amri kumi pamoja na maagizo mbalimbali kama kielelezo cha jinsi watakavyoishi kwa mahusiano mema kati yao na Mungu, na kati yao wenyewe. (Kut. 19:1 – 23:18). Baada ya kutoka utumwani Misri kwa nguvu za uwezo wa Mungu, walisahau yote Mungu aliyowatendea kwa kuwaongoza salama jangwani, akawalisha maji na chakula, akawashindia vita dhidi ya maadui wa makabila mbalimbali, na zaidi sana kuwapa na kuwamilikisha nchi ya ahadi ya Kaanani iliyokuwa na sifa zote za uzuri na utajiri. Wakavunja maagano yake kwa kukosa utii mbele za Mungu. Ingawa Mungu alikuwa na mamlaka juu yao (kwa maana ya kuwa mume au Bwana) lakini hawakujali. Wakawa wakiabudu miungu mingine.

Kwa kuvunja agano hilo, ilikuwa sawa na kuvunja mahusiano mema kati yao na Mungu ambao Mungu alipenda sana kuwa nao. Mungu akaondoa mikono yake ya ulinzi juu yao. Hivyo ikafika kipindi walipovamiwa na maadui toka Babeli, wakawapiga, wakawatesa, kisha wakawachukua utumwani kwao Babeli, walikotumikishwa takribabi miaka hamsini (50). Muda wote huo, hawakufurahia kamwe kukosekana kwa mahusiano mema na uwepo wa Mungu kati yao kama walivyokuwa wakifurahia mwanzo kabla ya kuvunjika kwa agano. Kwani miungu yao haikuweza kuwasaidia.

Kwa hiyo sasa, Mungu anaahidi kufanya agano jipya na watu hawa wa Yuda na Israel nzima. Anasema, agano hili halitakuwa kama lile la kwanza walilolivunja ambalo hawakuweza kumkaribia Mungu bila kuhani ambae aliruhusiwa kuingia patakatifu pa patakatifu ili kuombea watu msamaha wa dhambi zao kwa Mungu. Bali sasa, ataweka sheria yake ndani yao na kuiandika katika mioyo yao. Atakua Mungu wao, nao kuiandika katika mioyo yao. Atakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wake. Wala hawatahitaji kufundishana juu ya kumjua Mungu kwani wote wadogo kwa wakubwa watamjua. Maana atausamehe uovu wao na dhambi zao zote hatazikumbuka tena. (Yer. 31:34 na 33:8). Je! Ni agano la jinsi gani hili imara na lenye nguvu ya namna hii? Na ni lini lilitimia?

I. AGANO JIPYA NDIYE YESU KRISTO

Wapendwa wasomaji; ahadi za Mungu ni za kweli na ni amini. Wakati ule ulipowadia Mungu alitimiza ahadi yake kwa watu wake; kwa kulisimamisha agano jiypa kwa njia ya Yesu Kristo mwana wake wa pekee; alipozaliwa kwetu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Na kwa kifo chake akaleta upatanisho wa kweli kati yetu naye Mungu. (Ebr. 10:9b; 7:22; 9:15, Kol. 1:19 – 21)

Agano hili haliwezi kuharibiwa wala kuvunjwa tena na mapungufu ya wanadamu, kwa sababu baraka zake hazitategemea utiifu wa wanadamu kwa kuzingatia sheria kadha wa kadha. Bali Mungu mwenyewe atawabadilisha wanadamu kwa kufanya kazi ndani ya mioyo yao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Akiwapa watu wake ufahamu bora wa kuyafahamu mapenzi yake na pia nguvu ya kiroho ya kuwawezesha kuyatekeleza. Ndio maana katika ule mstari wa 34 anasema “ Wala hawatafundishana kila mtu na jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana, kwa maana watanijua wote tangu mdogo hata mkubwa miongoni mwao (Tazama pia Ebr. 8:11)

Badala ya kutegemea kuhani ili wamkaribie Mungu, yeye Yesu Kristo atakuwa mpatanishi kati yao na Mungu na kwa sababu hiyo Mungu mwenyewe atashughulika na dhambi zao akiondoa vizuizi na kila aina ya vikwazo na kuweka ushirika wa moja kwa moja naye Mungu. Ndio maana wakati wa kifo cha Yesu Kristo msalabani pazia la hekalu lilipasuka ambalo lilikuwa kama kiambaza kati ya watu na Mungu. Kitendo hicho cha pazia kupasuka kilikua ishara kamili kwamba uhusiano wa wanadamu na Mungu umerudishwa. (Mt. 27: 51, Ebr.10:19 – 21). Kwa njia hii unabii ulilitimia kwamba uovu wao umesamehewa na dhami zao Mungu hatazikumbuka tena.

II. KATIKA YESU KRISTO TUNASAMEHEWA DHAMBI ZETU

Ndugu zangu wasomaji, ni ukweli usiopingika kwamba Mungu ni Mtakatifu. Naye hutoa ushirika mzuri na kujenga mahusiano mema na wote wanaomkubali na kuyatimiza mapenzi yake katika kumwamini, kumtii na kumkubali Bwana Yesu Kristo ambaye kwake ametimiza ahadi yake ya kufanya agano jipya na watu wake. Katika majira haya ya majilio, yamewekwa kwa makusudi maalum na Kanisa ili kuandaa mioyo ya Wakristo waweze kukumbuka tendo kuu Mungu alilolifanya la ukombozi kwa nia ya kujenga mahusiano na ushirika mpya naye. Na hivyo watu wake wote wamfahamu, wapate kukombolewa toka mateso, utumwa wa dhambi na nguvu za shetani.

Kwa hiyo ndugu zangu wasomaji, Mungu hana furaha anapoona wenye mamlaka na madaraka makubwa katika dunia hii wakikanyaga kwa makusudi haki za wanyonge, watu maskini na wale wa chini yao bila hofu yoyote ya Mungu ndani mwao. Hakuna mtu asiyejua kuwa kukanyaga haki za wengine ni dhambi. Sheria hii iko mioyoni mwa watu wote toka wadogo hadi wakubwa. Ndio maana utaweza kuona hata kwa mtoto mchanga anapouma ziwa la mama yake wakati akinyonya, huduwaa na kutoa macho pima akitazama mama yake kwa kusubiri adhabu aidha kwa kufinywa, kugombezwa, kunyang’anywa ziwa au kuonywa kwa ukali. Anajua kabisa kwamba amekosa.

Mpendwa msomaji, kama unahusika kwa njia moja au nyingine katika kudhulumu haki za wengine kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini kwenye familia, unakumbushwa ujirikebishe. Umpokee Yesu Kristo anayekujia kwa upatanisho wa Mungu ili ufaidi baraka za kusamehewa uovu wako upate fursa ya kufurahia uhusiano mwema wa Mungu wako.

Jambo jingine mpendwa linalosikitisha ni jinsi ambavyo hali ya ubinafsi, kujilimbikizia mali kwa njia isiyo sahihi, na roho ya madaraka imekuwa kama donda ndugu lisilotibika kwa watu wengi katika dunia hii, jambo ambalo limeshusha sana utu wa wengi. Mauaji ya kukusudia yanaongezeka siku kwa siku, vita kati ya nchi na nchi, kabila na kabila, ndugu na ndugu, dini na dini, wizi wa kutumia silaha, ugomvi kati ya mume na mke, watoto na wazazi n.k.

Sheria ya kutoua iko imeandikwa mioyoni mwa watu wote lakini inavujwa na baadhi yetu kwa makusudi kabisa. Mpendwa msomaji; endapo na wewe upo miongoni mwa hao, au kwa njia fulani unachangia, chukua nafasi hii ya pekee leo ujisahihishe na Bwana wa Kanisa Yesu Kristo akujie, akusamehe uasi huo na kukupatanisha na Mungu Mwenyenzi upate kuishi naye maisha yenye furaha na amani. Hii ni pamoja na wale wote wenye chuki na ndugu yeyote, tamaa mbaya za mwili, kukosa uaminifu katika mali za wengine na hata kazini. Mungu hana furaha na tabia ya jinsi hii. Lakini tukizitubia dhambi zetu katika jina la Yesu Kristo, yeye ni mwaminifu na wa haki atatusafisha kabisa na wala hatazikumbuka tena.

Wapendwa, tuwe na maandalizi ya busara wakati huu wa majilio tusije tukajisahau tukazama kwenye maandalizi ya starehe za mwili, kula na kunywa, kuvaa na kujipamba kwa nje na anasa nyinginezo. Hizi ni furaha za juu juu tu na zenye mwisho wake. Lakini furaha ya kweli ni pamoja na Kristo Bwana wa Kanisa yaani mimi na wewe. Isa. 1:19 anasema, mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi.

Mwisho

Wakristo wote na watu wa dini zote katika dunia wanaitwa kumpokea, kumwamini, na kumkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na mtawala wa maisha yetu kwani ndiye pekee aletaye furaha ya kweli maishani mwetu aliyefanyika Agano Jipya kwa upatanisho wetu na Mungu muumba wetu. Kwa njia hii tutafurahia Krismasi vizuri kwa mioyo safi katika maisha haya na kisha katika uzima wa milele daima. Mambo haya si rahisi kwa nguvu na akili zetu wenyewe. Ila tukimwomba Mungu na kuamini mioyoni mwetu, yeye atatuwezesha kwa hakika. Na amani ya Kristo ipitayo akili zote iamue mioyoni mwetu sasa na hata milele. Amen.

Rev. Elishiisa W. Mbise,
Lutheran College of Theology Mwika
P.O. Box 3050 ,
MSOHI.
E-mail: mwika@elct.org

 

 

 


(top)