Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

JUMAPILI, NOVEMBA 26, 2006.
Siku ya Bwana ya Mwisho kabla ya Majilio.
Uzima wa Ulimwengu ujao.
Neno linatoka injili ya Yohana 5:24-29 na Mch. John Anderson Moshi
(->current sermons )


Utangulizi:

Injili ya kiroho kama Klementi wa Iskanderia (B.K. 150 -215) alivyoiita, ndiyo injili inayotofautiana na injili zingine tatu na inaonyesha kujifunua kwa Yesu Kristo katika ulimwengu. Hivyo sehemu kubwa ya mafundisho ya Yesu Kristo ni kumtambua yeye kama mwana wa Mungu na aliyetumwa kuleta ujumbe huu mkuu wa kinabii. Pia kutukumbusha kwamba Mungu bado anatupenda na anataka watu wote tuingie katika uzima wa milele. Sisi wanadamu tumepewa uhai na Mungu na kwamba tunatakiwa tutunze uhai huo ambao ni thamani kubwa kwetu. Tukiangalia miili tuliyo nayo, uwezo wetu wa kufikiri na hata yale tunayofikiri na kuyafanya hasa yanayoonekana, ni uthibitisho kuwa kuna kitu kikubwa sana ambacho Mungu ameweka ndani yetu cha thamani kubwa.

Kuna mambo kadha wa kadha ambayo nafikiri ingefaa kuyaangalia kuhusiana na somo lililopo hapo juu.

1. KUTAMBUA THAMANI YA UHAI NA UZIMA MUNGU ALIOTUPA.

Mungu anatupenda kiasi cha kutufanya viumbe wa kipekee sana. Laiti wanadamu wote wangefahamu jambo hili, hapa duniani pangekuwa mahali pazuri na salama sana pa kuishi, pia mahali ambapo Mungu angeendelea kushuka na kuzungumza na sisi watoto wake, pengine kuliko ilivyo hivi sasa. Kwani maneno yake Matakatifu kutoka Yohana Mt. 3: 16 yamedhihirisha hilo. Hata kuimarika kwa imani kungekuwa katika kiwango kikubwa mno. Yesu akiwa kwenye mjadala mzito na wayahudi wakimpinga kupitia huduma alizokuwa anafanya, anawafafanulia kwamba uzima wa milele unapatikana kwa kulisikia neno na kulitii. Pia anawasisitizia wamwamini yeye kwani ndiye aliyetumwa na Mungu mwenyewe, hawataingia hukumuni. Hapa alikuwa anawataka wayahudi watambue kwamba uhai na uzima wa milele watoka kwa Mungu na mwana wake Yesu Kristo amekuja kufundisha hivyo ili watu wote waelewe wakiwemo wayahudi.

2. KUSIKIA NENO NA KULIAMINI (mst. 24-25).

Yesu anaendelea kusisitiza kuwepo kwa saa na kuja kwa saa ambayo wafu wakisikia watakuwa hai. Pengine yaweza kuwa ngumu kuamini maneno haya ya mstari wa 25, lakini maneno yaliyoko katika Mathayo 8:22, yanaonyesha mmoja wa wanafunzi wake alipotaka kumfuata lakini akawa na udhuru wa kutaka kumzika baba yake!! Na Yesu hapa alimtaka amfuate na awaache wafu wazike wafu wao!! Pengine alitaka waelewe kwamba wakati wakiwa hai walipaswa kulisikia neno la Mungu na kuliamini. Lakini wayahudi wanaonyeshwa kuwa, kuna nafasi kwa mfu kusikiliza sauti ya Mwana wa Mungu. Imani haiwezi kujengeka pasipo kuelewa na kuipokea sauti ya Mungu ambayo ndiyo msisitizo wa Yesu Kristo. Hata hivyo, uhai Yesu anautaka kwa watu wote, kwamba wamezikwa makaburini au wana uhai huu wa nyama, hiyo kwake si kitu. Thamani ya wote ni kubwa na inazingatiwa. Swala kubwa hapa ni kama mwanadamu ameisikia sauti ya mwana wa Mungu na kuifuata. Wayahudi walikuwa na tatizo la kufungwa na sheria zaidi kuliko kumfuata na kumsikiliza Yesu Kristo. Walifikiri Yesu yuko kinadharia tu na mafundisho yake ni ya kizushi!! Pia hawakuamini kwamba ndiye masihi aliyetabiriwa na manabii hapo kwanza. Pamoja na kushuhudia miujiza na huduma mbalimbali ambazo Yesu alifanya mbele yao, bado mioyo yao ilikuwa migumu sana. Ndiyo maana Yesu alisisitiza sana juu ya uzima wa nafsi, alitaka wayahudi wazichunguze sana nafsi zao.

3. UHAI LAZIMA ULETE UZIMA WA NAFSI (mst. 26).

Yesu alifundisha kwa kusema, mtu akiipenda nafsi yake, ataipoteza. Lakini mtu akiichukia nafsi yake kwa ajili ya Yesu Kristo, huyo ataiponya. Mtu anaporidhisha nafsi yake kwa vile vitu anavyovipenda hata kama vinadhuru mwili mradi tu anavipenda, kuna uwezekano wa kungamiza mwili na roho. Lakini yule anayejali zaidi mafundisho ya neno la Mungu bila tamaa zinazovutwa na mwili, pia kujizuia sana na mvuto unaotokana na msukumo wa ndani ya mwili, basi huyo aweza kujikinga na mambo mengi yanayoweza kuhatarisha nafsi na mwili wake, na hivyo akawa salama zaidi. Yesu anawataka na kuwafundisha wayahudi wazichukie nafsi zao ili waweze kuziponya. Waachane na tamaa za kimwili ambazo zaweza kuharibu mwili na nafsi zao. Kwa kuwa mwelekeo wao ulikuwa ni kutetea mambo yao, Yesu alionyesha ukali kwao na msimamo kutetea mapenzi ya Baba wa mbinguni. Mapenzi ya Mungu ni kwamba wote wawe na uzima kama Mwana alivyo na uzima na Baba. Uzima unaotakiwa kwao ni wa kufa na kutopotea, si wa kufa na kupotea. Hata kama utakuwa umekufa, utafufuliwa na kuingia uzima wa milele, Yohana 8: 51 anadhibitisha hayo kwa yule anayelishika neno la Mungu.

4. IKIWA WAFU WATASIKIA SAUTI, JE, WALIO HAI?

Inawezekana kushangaa kidogo kusoma Yesu akisema wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, watakuwa hai. Twaweza kuwa na maswali mengi kuhusu huko waliko wafu na ikiwa wanasikia tena. Kwa waafrika halitakuwa jambo la kushangaza kwani imani ya kiafrika, itakubaliana na kauli ya walipo wafu kwamba wanaweza kuisikia sauti kule wanakokwenda. Imani hiyo inatuonyesha kwamba wanaokufa hawapotei moja kwa moja bali kuna mahali fulani ambapo wanawekwa kusubiri kiama yao. Swali kubwa hapa ni kama hawa wafu wataisikia sauti ya neno la Mungu na kulipokea neno hilo na kisha kufufuliwa na kuwa hai tena tayari kwa uzima wa milele, walio hai wameziba masikio? Kwani walio hai wanawaona wahubiri na wanajua sauti inakotokea, pia wako na wahubiri hawa muda wote wa uhai wao! Yesu hapa, anataka wayahudi waelewe jambo hili muhimu. Ni ukweli usiopingika kwamba imani inakuja kwa njia ya kusikia na kusikia kwaja kwa njia ya neno, asiyesikia neno, hawezi kuelewa na kutoelewa hakuwezi kuimarisha imani ya mtu. Kwa kuwa wayahudi walikuwa wabishi sana, na walikuwa na misimamo yao, Yesu aliwaonyesha kuwa hata kama watakufa, watatambulika wenye heri au laana. Yaani walilisikia neno wakawa hai, au walilidharau neno wakafa na kupotea. Yesu atahakikisha haki ya kila mtu imepatikana, wote wakiwa hai, itakuwa furaha mbinguni lakini wakiwepo wafu waliokataa neno, hawa watahukumiwa. Yeye amepewa mamlaka na amri ya kuhukumu. Ndiyo maana anawaambia wayahudi wasistaajabie maneno hayo kwani muda huo unakuja kwa hakika. Na kwamba waliofanya mema, watafufuliwa kwa maisha ya uzima na waliofanya mabaya, watafufuliwa ili wahukumiwe.

5. FUNDISHO LA SOMO.

Maneno haya aliyasema Yesu Kristo wakati ule akiwafundisha wayahudi na jamii iliyokuwepo wakati huo ielewe. Hata kizazi hiki leo kinafundishwa maneno hayo kwani neema ya Mungu bado ingalipo kwa wote na wote wanaoamini ili nao wapokee uzima wa milele. Ninachokiona hapa ni kwamba si lazima tufikie hatua ya kubishana na Yesu kama wayahudi ndipo tuonywe kwa ukali. Lakini maisha yetu yaweza kuwa kielelezo cha kutosha kumtukuza shetani na kumpinga Yesu hata kuwazidi wayahudi. Au kuwa kielelezo cha kutosha kutupatia uzima wa milele. Swala si kwamba tumeshaondoka, bali swala kubwa hapa ni wapi tunakokwenda hasa. Je, tuna hakika na safari yetu kwamba tunakokwenda tutamkuta Yesu huko na atatukaribisha? Hakuna mahali pengine pa kutengeneza maisha yetu ila ni wakati huu ambapo tuna uhai huu wa mwili. Wakati huu neno la Mungu linahubiriwa kwa nguvu sana ndipo ambapo tunatakiwa kulisikia neno na kulitenda ili kuwa waumini wa kweli wa neno. Lengo la Mungu wetu ni lilelile kwamba wote wawe na uzima. Mungu bado hajakata tama na sisi, anataka tubadilike hasa pale tunapokwenda kinyume na mapenzi yake. Mungu amemtuma mwana wake wa pekee ni tupate uzima kwa yeye. Katika injili ya Yohana 1: 4 tunasoma, “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu”. Hapa tunafundishwa kwamba mahali pa kuupata uzima ni kwa Yesu Kristo pekee, maana ndiye tuliyepewa na ndiye tunayepaswa kumuangalia na kumsikia ili tupate uzima.

Tunapotafakari sana juu ya maisha yetu yajayo, tutafakari hasa juu ya uzima wa milele ambao Mungu mwenyewe anapenda na sisi tuwepo. Hapendi hata mmoja wetu apotee, tunadhibitishiwa haya katika Yohana 3: 16, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”. Yesu alikuja kutimiza mpango huo mzuri wa Mungu, yaani kuhakikisha hakuna hata mmoja atakayepotea. Lakini kila atakayesikia ujumbe huu wa Yesu, asiamini, huyo atapotea, ndiyo maana Yesu mwenyewe alikazana sana kufundisha akijua kwamba ni wajibu aliopewa na Baba yake wa mbinguni na anautimiza kikamilifu. Mimi niliyepata nafasi ya kukumbusha maneno haya, niwasisitizie kwamba ujumbe na wajibu wa Yesu bado umesimama palepale na tena mpango wa Mungu ni uleule. Ndiyo maana neno linasema, Yesu ni yule jana, leo na hata milele. Yesu anasema na sisi hata leo juu ya safari yetu. Tumekwishaanza safari, lakini ya kwenda wapi? Kila mmoja anapaswa kufahamu safari yake ni ya kwenda wapi. Zipo sehemu mbili tu za kwenda! Ama uzima wa milele au jehanamu ya milele. Tukumbuke kwamba Yesu amepewa mamlaka ya kutuhukumu, katika kitabu cha nabii Daniel 7: 10, 14, tunaelezwa habari za hukumu na mamlaka ambazohazitaangamizwa kamwe. Hivyo wapendwa tunakumbushwa kujiandaa kwa ajili ya maisha ya milele na kuyawazia hayo kwani ndivyo Mungu wetu anavyotaka tufanye. Hakuna namna nyingine ya kufanya kama sio kujiandaa mapema na kuweka mawazo yetu katika maisha yajayo.

Katika yote tunapaswa kuzingatia mambo matatu ili yatuwezeshe kuuona uzima wa milele. Kwanza, ni maisha yetu yatawaliwe na upendo kwa Mungu na kwa jirani zetu, pia tuwe na amani na furaha ili kuimarisha mahusiano yetu sisi na Mungu wetu wa mbinguni na majirani zetu, kupitia hali hiyo watu watafurahi na kumtukuza. Pili, maisha yetu yawe ya uvumilivu, yenye utu na fadhili ili watu wote tunaoishi nao wauige ukristo wetu na waone kweli tunamfuata Kristo kama yeye mwenyewe alivyosema. Tatu, sisi wenyewe tuwe mashahidi wa Kristo kwa kuwa waaminifu, wapole na wenye kiasi. Hapa wengine watakapotuona wamwone Kristo ndani yetu. Mtume Paulo amesisitiza sana maneno haya katika waraka aliowaandikia Wagalatia.

Lakini mambo haya hayawezi kutokea tu kama jua linavyoweza kutokea asubuhi bila kuitwa! Lazima watu wasome neno la Mungu kwa nguvu zote, neno ndilo laweza kutuzalia tabia hizi nzuri ambazo kwa muda wote zitamtukuza Mungu. Neno ndilo linaimarisha imani yetu kwa Yesu na hata kutambua uwepo wa nguvu ya Mungu kwetu. Hata hivyo sisi wenyewe hatuwezi kupata roho ya kutambua nini tufanye pasipo uwezo wa Yesu mwenyewe na uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu kuingia ndani yetu na kutuwezesha. Hivyo yapasa sisi kuona hitaji la kukaa na Yesu na hivyo tuonyeshe roho ya unyenyekevu na ya uhitaji ili tufunguke na kuwa na hamu ya kusoma neno la Mungu kwa nguvu. Tutakapoisikia sauti hiyo nzuri na inayotuita kwenda kwa yesu, basi tutaimarika kiimani na mwisho tutaingia katika uzima ule wa milele. Mungu atubariki sisi sote. Amen.

Mchg. John Anderson Moshi,
Chuo cha Theologia na Uinjilisti Mwika,
Moshi – Tanzania.
johnmoshi@yahoo.com
Mwika@elct.org

 

 


(top)