Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

TRINITY 20, OCTOBER 29, 2006
A SERMON ON LUKE 6:27 – 38 (KISWAHILI) BY DAWSON CHAO
(->current sermons )


“IWENI NA HURUMA KAMA BABA YENU WA MBINGUNI”

Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu,watendeeni
mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao
wawalaani ninyi, wao mbeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye
shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyae joho yako, usimzuilie na
kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyae vitu vyako, usitake
akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeeni
vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha
fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.
Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani?
Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini
kupata kitu kwao mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha
wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile.
Basi wapendeni adui zenu, tendeni mema,
na kukopesha msituaini kupata malipo, na thawabu yetu itakuwa nyingi; nanyi
mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na
waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu,
nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi
mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo hicho cha kujaa na
kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa
vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtachopimiwa. (Union Version)



Kusudi:
Wote wajue kwamba, kile usichotaka kutendewa na wengine usitende. Na kama tunavyotaka watu wengine watutendee sisi, tuwatendee wengine mambo haya.

Utangulizi: Kuna msemo wa Kiswahili kuwa, mtoto akipenda/akililia kisu mpatie na ala yake. Kwa kichaga (watu wanaoishi Kilimanjaro) usemi huo ni kuwa “mtoto wa mfalme (Mangi) akipenda kutamani kisu chako mpatie na hiyo ala yake. Msemo huu unaacha maswali mengi, Je anahitaji kwa nini? Atarudisha baada ya kutumia? Au je, atatumia kwa namna gani, kwa kusudi jema au baya? Katika somo hili kuna maswali pia ya kujiuliza ambayo ni Yesu peke yake mwenye majibu sahihi, mfano wapendeni adui zenu (b) Mpe kila akuombaye na akunyang’anyae vitu vyako. (c) Akupigaye shavu moja, mgeuzie na la pili? Msihukumu nk. Katika somo la leo tutajaribu kutafakari ili kuona kama Yesu anatufundisha nini katika neno hili.


WAPENDENI ADUI ZENU, WATENDEENI MEMA WALE
WANAOWACHUKIA, WABARIKINI, MSIWALAANI
.

Hili ni jambo gumu peke yetu pasipo msaada wa kimungu hatuwezi. Ni sehemu ya hotuba ya Yesu iitwayo hotuba ya mlimani, mahubiri ambayo nia yake ni kuonyesha njia inayopasa kwa wafuasi wake Yesu Kristo.
Hiyo inatudai kuwa tayari kufanana na Kristo aliyetuita na kututaka tuweze kuwaona watu wengine, kuwajali na hata kuwachukulia kama kwa Huruma ya Kimungu, yamkini hata na wale ambao wanataka kutuonea na kutudhulumu wataguswa. (Mt. 5: 17 – 48)
Jirani yangu mmoja ametamani sehemu ndogo ya shamba langu, iende upande wake. Tumetenganishwa na barabara lakini anatamani kuvuka barabara ile na kudai sehemu iliyo kwangu ya kwamba ni mali yake. Katika taratibu za mila zetu kuna mti unaoitwa “sale” ambao ndio unaooteshwa kuonyesha mpaka. Huyu jirani amekwenda akaotesha mti huo bila ya ridhaa yangu. Sote ni Wakristo, madhehebu tofauti. Mimi ni mtumishi wa Kanisa, Biblia imekataza tusipangue na kusogeza mpaka wa kale, lakini ndugu jirani huyu haonyeshi kujali, hata pamoja na mimi kumwona kipekee katika hali kama hiyo. Nimeamua kukaa kimya na kutofuatilia zaidi katika hatua zaidi za kisheria. Nimeacha aendelee kukidhi tamaa yake baada ya kuona bado tu anang’ang’ania sehemu iliyo yangu. Kwangu mimi nimesema hivi: Ardhi na vyote ni mali ya Mungu, ikiwa sehemu anayodai ni mali yake itamkaa kwani anayegawa haki ni Mungu. Atayafurahia matunda yake. Lakini ikiwa amenidhulumu haitamkaa itarudi kwangu kwani anayehukumu kwa haki ni Mungu peke yake.


Sitaki kujidai kwamba nimetimiza wito wa Yesu katika mstari 27 – 30 kwani ukweli ni kuwa madai ya ukamilifu wa Mungu ni zaidi ya binadamu anavyoweza kutekeleza peke yake pasipo msaada wa kimungu. Ndio maana Yohana Mzee katika Waraka wake anatuonya sisi tulio wafuasi wake Kristo akisema ya kwamba, “Tukisema kwamba hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani mwetu…” Tukisema kwamba hatukutenda dhambi twamfanya yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu (I Yoh. 1:8,10). Ndugu yangu nakiri pia kwamba mimi siyo mkamilifu. Ni mdhambi aliyesamehewa kwa neema yake Kristo tu. Katika kisa nilichoeleza hapo juu nilichojaribu kufanya ni kukubali unyonge na kumwachia yeye aliye na uweza na nguvu za kutuwezesha sisi sote, mimi na jirani yangu kupata haki (Fil. 4:13); (Rum 14: 17). Yeye ni mwenye haki naye anatuhesabia haki kwa imani ya Yesu Kristo. Tena haki huinua Taifa bali dhambi ni aibu ya wote. (Mith. 14:34). Tukitambua hivyo upungufu wetu kama binadamu yatubidi kutubu kwani yeye ni mwaminifu. Tukiungama atatusamehe kabisa. ( 1Yn. 1:9


TUSIDHARAULIANE NA KUHUKUMIANA, TUMWANGALIE KRISTO

Sisi wakristo tumeitwa, tumealikwa na Mungu ili tuingie katika ufalme wake kwa kumwamini Yesu Kristo mwanae pekee aliyetufia msalabani, damu yake ikamwagika na siku ya tatu akafufuka kwa ajili yetu. Yesu ndiye mwanakondoo wa upatanisho azichukuaye dhambi zetu. (Yn. 1:29). Basi tusidharauliane sisi kwa sisi na kujidai kuwa watu bora kupita wengine. Hatuna la kujivunia kwani wokovu tumepewa kwa neema tu. Hakuna anayestahili mwenyewe pasipo msaada wa Yesu Kristo. Hebu tazama amri za Mungu amri kumi (10) si zinatuhukumu? Nani anaweza kutimiza zote? Kadhalika rejea mahubiri (hotuba) ya Yesu mlimani kama inavyoonekana katika Mathayo 5 – 7 au ilivyo hapo juu kwa Luka, kifungu tulichosoma, nani ameweza kutimiza? Basi tusichokozane, bali tuheshimiane na tuombeane! “…kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu, kila mtu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu”. Je, wewe unakumbuka taarifa zako?
Hebu tukumbuke sisi wakristo tulichoitiwa ni kumpokea Yesu Kristo, kumwamini na kumfuata Yesu ndiye njia ya kutufikisha katika ufalme wa Mungu. Yeye Yesu ni njia kweli na uzima (Yn. 14:6) Tumwangalie Mungu aliyetupenda upeo hata tulipokua wafu kwa sababu ya dhambi alimtoa Yesu Kristo kufa na kuwa fidia yetu akatukomboa ili sisi tusipatikane tena na hatia ya hukumu ya kifo (Rum. 8: 1 – 4). Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki (Rum 10:4f). Musa aliandika juu ya haki iokoayo kwa kufuata sheria. Lakini Kristo ametuokoa kwa imani tu. Tusijivune bali tuogope (Rum. 11:20c) Tumche Mungu na kumtegemea kuliko vitu vingine vyote.


MAISHA MAPYA KATIKA KRISTO YANA USHUHUDA MZURI

Biblia inatufundisha kwamba mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya ya kale yamepita tazama yamekuwa mapya (2Kor. 5:17). Sasa sisi Wakristo tu wajumbe wa Kristo na kwa ajili ya Kristo, tukatende kazi pamoja naye. Yesu amejitolea kwa upendo mkuu ili sisi tupate kupona (Yoh. 3:16) Yeye asiye na dhambi alifanywa kuwa dhambi, kwa ajili yetu (2Kor. 5:21). Tunatangaza habari hizi njema kwa watu wote. Yesu anawapenda watu wote wafikilie wokovu na kuingia katika ufalme wa Mungu. Sisi wakristo ni wasemaji na watendakazi pamoja na Yesu, tukiishuhudia Injili kwa watu wote wa makabila yote na mataifa yote na dini zote. Yesu ni mfalme, na Yesu anaokoa.

Katika ushuhuda wetu tuangalie, tujihadhari tusiwakwaze wenzetu hata kama ni wa imani tofauti. Nuru yetu na iangaze watu wote waone matunda ya imani mpya katika Kristo na kumtukuza Mungu ( Mt. 5:16) Iman itendayo kazi kwa upendo ni ushuhuda mzuri. Ufalme wa Mungu, Biblia yatuambia si katika kula na kunywa, bali ni kutenda haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu (Rum.14:17) “ Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena hukubaliwa na wanadamu (Rum. 14:18). Mungu anapenda kutumia nafasi zetu na sauti zetu kutangaza habari njema/ ujumbe wake kwa njia mbalimbali. Tena sauti zetu Wakristo zitoe unabii na utetezi kwa wanyonge, mfano Walio wajane, maskini, wenye Ukimwi, walemavu nk. Sauti zikemee vitendo viovu katika jamii yetu kama rushwa, ufisadi serikalini na kanisani na katika jamii kwa ujumla. Tusipoinua sauti, bwana atainua mawe (wasiotajwa) nao watashuhudia.

Onyo
: Tumepewa bure, lakini tusipokee neema hiyo na kuishi bure bila kuzalisha kazi na matendo yanayoshuhudia neema ndani mwetu. Sisi tu watenda kazi pamoja naye Yesu katika maisha mapya ( 2Kol. 5:20). Hayo maisha mapya yanatusukuma tuwe na upendo na huruma kama yeye alivyo. Ni maisha yenye utu uliojaa, unaothamini na kutanguliza wengine “Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi watendeeni vivyo hivyo.” Ni kama kusema, usilotaka tendewa usitende; yaani umjali na kumpenda mwenzio kama nafsi yako. (Lk.6:31,Mt.7:12). Tukumbuke Yesu alisema katika Biblia kuna amri mbili kuu (a) Kumpenda Mungu … (b) Kupenda jirani kama nafsi yako, katika hizo ndio jumlisho ya Torathi yote na mafundisho ya Manabii. Huu ndio ukamilifu.


MWISHO
Katika msemo nilioanza nao, mtoto ukimpa kisu na ala yake, wala hukuzuia kitu, lakini kuna uwezekano kikamkata naye akajifunza baada ya kuumia (b) Katika mfano wa hotuba ya Yesu tunaweza pia kutegemea kwamba aliyeachiwa kanzu huenda ikamvuta rohoni, au akazomewa na wengine ikamkosesha amani na kurudisha. (c) Lakini mfano wa Yesu mwenyewe, yeye ndiye jibu kamili kwani alijitoa yeye kweli nafsi yake kuwa fidia ya wengi. Alijinyenyekesha akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba (Filp. 2:8) ili sisi tusihukumiwe tena. Ni huruma tu, hatukustahili.
Basi tuyatende yote kwa upendo pasipo mashindano wala manung’uniko tupate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, bali wenye huruma kama baba yetu wa mbinguni alivyo. (Filip. 2:14). Yeye huwapa watu wote mahitaji yao, zaidi sana wale walioitwa kwa kusudi lake.

Rev. Dawson E. Chao
Lutheran College of Theology Mwika
P.O. Box 3050,
MOSHI.
E-mail: mwika@elct.org
dawsonchao@yahoo.com



(top)