Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

UTATU 19, OKTOBA 22, 2006
MAHUBIRI NA MCH. ELIA M. MANDE KUTOKA MARKO 5:25-33
(->current sermons )


Ndugu mpendwa, Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo katika kufundisha na kuhubiri kwake Habari Njema za Ufalme wa mbinguni pia alitenda miujiza. Alifufua wafu na hata aliponya wagonjwa ambao waliteseka kwa miaka mingi kwa tiba mbalimbali na kwa gharama kubwa bila ya kupona.

Matendo hayo makuu ya miujiza yalithibitisha kwamba Ufalme wa Mungu u-ndani ya watu wake. Ufalme wa Mungu u-ndani ya watu wake waliompokea Kristo Yesu mioyoni mwao na maishani mwao. Maana Kristo Yesu mwenyewe anasisitiza, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yn. 14:6. Na popote alipokwenda Yesu, alitenda mema na maelfu ya watu walimwendea na kumfuata.

APONYWA KWA KUGUSA VAZI LA KRISTO
Katika somo hili Bwana Yesu alikuwa anakwenda nyumbani kwa Yairo, mmoja wa maofisa wa Sinagogi ili kumponya binnti yake aliyekuwa mgonjwa hoi taabani. Umati mkubwa wa watu walimfuata, Mwanamke mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu muda wa miaka kumi na miwili, alipata habari zake kwamba Bwana Yesu anapita, hivyo alikwenda moja kwa moja kwenye umati huo ili apate nafasi ya kumwendea Bwana Yesu aponywe ugonjwa wake huo uliomhangaisha na kumtesa kwa miaka mingi. Kweli alikuwa ameteseka sana. Na aliingia gharama kubwa akitafuta matibabu kwa waganga mbalimbali bila ya mafanikio yo yote. Pamoja na mateso na mahangaiko hayo yote lakini hakukata tamaa. Bado alikuwa na imani na tumaini kwamba Bwana Mungu yupo na kwa huruma yake atasikia kilio chake na kumponya siku moja. Mara nyingi nasi katika maisha haya tunakumbana na magonjwa na shida mbalimbali kiasi kwamba wengine huvunjika moyo na kukosa matumaini na hata kuiacha imani.

Mwanamke huyu alidumu katika imani na tumaini katika Bwana Mungu. Kumbe! Siku hiyo sasa ilikuwa imewadia. Wakati ulikuwa umefika na kupokea uponyaji, kupokea mujiza wa uponyaji wake kwa msingi wa imani.

Mpendwa, ona imani ya huyu mwanamke, Umati mkubwa wa watu ulimsonga mno Bwana Yesu na ilikuwa vigumu yeye kusema neno kwa Bwana Yesu. Lakini bado alisukumwa na imani na tumaini kwamba hata angegusa tu mavazi yake Kristo angepona ugonjwa wake. Hapa nasi leo tunajifunza neno muhimu. Tunapata neno la kuweka moyoni mwetu. Wakati wote tunapopata shida ya aina yo yote ile, tuwe na moyo mkuu kumwendea Bwana Yesu. Tuwe na moyo mkuu kumwendea Bwana Yesu kwa mahitaji yetu mbalimbali ya kiroho na kimwili naye atatujibu sawaswa na mapenzi yake na kwa wakati wake.

IMANI HUPONYA NA HUOKOA
Mwanamke huyo aliwaza moyoni mwake, “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.” Mk. 5:28. Kweli kwa imani alifanya hivyo. Neno linasema alipogusa tu mavazi yake, mara chemchem ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba kweli amepona. Bwana Yesu asifiwe! Yeye ni Mwokozi wetu na Mganga wetu Mkuu! Anaponya na anaokoa roho za watu. Katika uponyaji huu wa ajabu tunaona jambo lingine la kustaajabisha. Nalo ni hili: Bwana Yesu alifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka. Aligeuka kati ya mkutnao na kuuliza, “Ni nani aliyenigusa mavazi yangu?” Kwa msingi wa swali hili inathibitisha wazi kuwa Yesu Kristo hakuwa mwanadamu tu. Yeye alikuwa mwanadamu kweli na Mungu kweli. Alikuwa na nguvu za kimungu na ndiyo maana hata mavazi yake yalikuwa na nguvu za uponyaji. Tena alikuwa na ufahamu wa kimungu: Alifahamu yote na hakuna lisilowezekana kwake. Kwake Yesu Kristo yote yanawezekana.

Wanafunzi wake walishangaa sana kwa nini aliuliza swali hilo. Wakasema jinsi umati wa watu ulivyomsonga-songa, inawezekanaje kumfahamu yule aliyemgusa? Lakini yule mwanamke aliingiwa na hofu na kutetemeka. Alikuja kwa Bwana Yesu na kumwangukia na kumweleza kweli yote.

Ndivyo! Hata nasi leo tunapomwendea Bwana, tumwendee kwa mioyo iliyopondeka. Tumwendee kwa mioyo ya hofu na kutetemeka naye hakika atajibu maombi na sala zetu. Tumwendee kwa mioyo ya unyenyekevu naye atatuponya magonjwa yetu yote ya kiroho na kimwili. Tena yatupasa tumwangukie kama alivyofanya huyo mwanamke na kwa hakika kwa kufanya hivyo nasi tutapona katika maisha haya na hata katika ulimwengu ujao.

SISI JE! TUTAPATAJE KUPONA?
Ndugu mpendwa, hilo ni swali muhimu kwa kila mwanadamu kujiuliza. Ni swali muhimu kwangu mini na kwako wewe mpendwa unayepokea ujumbe huu kujiuliza. Katika Waebrania 2:3, Neno la Mungu linaleta ujumbe huo kuwa sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii?

Wakati wa wokovu wetu ni sasa. Saa ya kupona kwetu ni leo. Mtume Paulo anasema, “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.” Ndipo anasisitiza ujumbe huu kwa nguvu, (Kwa maana anasema),

“Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu
nalikusaidia, tazama, wakati uliokubalika ndio sasa, tazama,
siku ya wokovu ndiyo sasa) 2Kor. 6:1-2.”

Katika mkutnao mmoja wa Injili miaka ya hivi karibuni nilishuhudia mujiza wa Bwana Mungu wa uponyaji na baraka ya mtoto kwa mara ya kwanza kwa ndoa ya miaka saba. Kabla ya maombezi, mtu na mkewe walieleza jinsi walivyohangaika na kuteseka kwa miaka saba bila kupata mtoto katika ndoa yao. Walifika katika hospitali mbalimbali za serikali na za binafsi. Madaktari walisema mama alikuwa na shida kiuoni na wasingeweza kupata mtoto labda kwa maombi tu.

Nakumbuka vema, baada ya maombezi na baada ya miezi minne mama huyo alikuwa mja mzito kwa mara ya kwanza katika ndoa yao na baada ya miezi tisa alijiungua mtoto wa kike aliyebatizwa kwa jina, Pendo. Kristo Yesu alimponya huyo mama na kubariki ndoa hiyo kipekee wakapata mtoto wao wa kwanza katika ndoa yao ya miaka saba.

Walifika mbele za Bwana katika maombezi hayo wakiwa na imani kwamba Bwana Yesu anaponya na anaokoa. Kabla, walishuhudia wao wenyewe kuwa Bwana Yesu aliokuwa hapa duniani alihubiri na kufundisha Neno la mungu katika miji na vijiji. Katika kuhubiri na kufundisha huko aliponya wagonjwa mbalimbali. Nao waliamini Bwana atawapa uponyaji wake na hata kubariki ndoa yao kupata watoto. Ndivyo ilivyotokea. Jina la Bwana Mungu na lihimidiwe.

Ndugu mpendwa, yawezekana nawe hivi leo unapopokea ujumbe huu una ugonjwa unaokusumbua ama hitaji maalum katika maisha yako. Bwana Yesu yu tayari kukuponya kama alivyofanya kwa huyo mwanamke. Bwana yu tayari kukupa wokovu iwapo utamkaribisha moyoni mwako kwa imani.

Imani yako katika Kristo itakuponya na kukuokoa, uwe na amani na uwe mzima katika Kristo Bwana wetu, sasa na hata uzima wa milele katika ufalme wa mbinguni.

Naye Kristo Yesu Mwokozi wa ulimwengu anabisha hodi moyoni mwako na maishani mwako umfungulie mlango na umkaribishe. “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha, mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” (Uf. 3:20-21).

AMIN.


Mch. Elia M. Mande,
Chuo cha Biblia na Theologia Mwika,
S.L.P. 3050,
Moshi - Tanzania
E-mail: mwika@elct.org

 


(top)