Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

JUMAPILI, OKTOBA 8, 2006
Siku ya Bwana ya 17 baada ya Utatu.
Neno linatoka Injili ya Marko 2:23 – 28 na Mch. John Moshi
(->current sermons )


UHURU WA MKRISTO

Utangulizi:

Mtu yeyote anayeitwa mkristo, anatajwa kwa jina la Kristo, hivyo hana haja ya kuwa na mashaka juu ya ukristo wake. Kila mtu atakubaliana nami kuwa asiyekuwa mkristo ndiye mwenye mashaka makubwa kwa sababu tumaini lake liko katika jambo fulani. Kwa mkristto ni tofauti kabisa.

Dhambi ilipoingia duniani, ilimuathiri na mkristo pia. Kwa hakika hakuwa na njia ya kufanya kwa kuwa ni mtu kama watu wengine. Tatizo hapa ni kushindwa kutumia ukristo wetu vizuri. Kama mkristo amemvaa Kristo vizuri hana budi kushinda kila aina ya jaribu linalokuja mbele yake kama mkristo. Ukristo ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Anayekuwa mkristo ni lazima ayawaze hayo! Lakini ni wangapi ambao ni wakristo wanaweza kufanya hivyo? Wanaweza kuwa ni wachache sana!! Kwa nini, pengine ni ajabu sana kusema mkristo ni mtumwa wa dhambi. Haipaswi kabisa kusema hivyo. Hata Yesu mwenyewe atashangaa sana. Mkristo ameingiaje tena kwenye utumwa wa dhambi? Ajabu hapa mtu ni mkristo kwa jina, lakini utumishi ni kwa shetani au mchanganyiko.

Utumwa wa dhambi unakuja pale mtu anapokuwa mtumishi wa shetani moja kwa moja. Hata mkristo anaweza kuwa mtumwa wa dhambi. Mazingira mwanadamu anayoishi sasa hivi, anaweza kuwa kwenye hali hiyo kama hakuwa makini na ukristo wake. Wakristo wengi wameingia kwenye maisha yaliyo kinyume na mpango wa Mungu na kuuzoea mpango huo pasipo kujua kwamba wameshatekwa na kuwa watumwa wa shetani na kuwa hawana uhuru ambao Yesu aliuleta kwetu kwa njia ya kifo cha msalaba.

Yesu alisema kwamba yeye ni nuru itakayoangaza kila mahali. Nuru hii ni neema pekee ya kumtoa mwanadamu kutoka kwenye giza la utumwa wa dhambi na kumuingiza katika nuru ya wokovu, yaani kuwa huru. Hapa ukristo una maana kubwa. Yesu anajibu swali la mafarisayo baada ya wanafunzi wa Yesu kuonekana mashambani wakivunja masuke siku ya sabato. Kwa mafarisayo, sheria haiwaruhusu kufanya kazi kama hiyo siku ya sabato, lakini kwa Yesu na wanafunzi wake, wako huru kufanya mradi wana haja ya kweli na hitaji la kweli. Hawa hawafungwi na sheria ya kisabato. Yesu anawakumbusha vizuri jinsi Daudi akizijua vizuri sheria za kikuhani alivyoingia hekaluni na kuanza kuila mikate isiyotakiwa kuliwa, isipokuwa na makuhani tu, alipokuwa na haja na njaa yeye pamojja na wenziwe. Hitimisho la mfano wa Yesu kwa mafarisayo ni kuwa, pale hitaji linapotokea, linashughulikiwa mara moja bila kujali kuwa ni siku gani linatokea. Vinginevyo mtu akiwa katika udhaifu hawezi kutimiza wajibu wake sawasawa!

Hata hivyo Yesu anataka kuonyesha pia kwamba kuja kwake hakumuweki tena mwanadamu chini ya sheria bali kunamuweka huru kama akikubali kuupokea wokovu ulioletwa naye kwa njia ya kifo cha msalaba. Huu ni mpango wa Mungu kwamba mwanadamu aondoke kwenye utumwa wa dhambi na kuwa huru ndani ya Yesu Kristo mwenyewe. Mwanadamu anakuwa chini ya mamlaka shetani kwa njia nyingi. Ndani ya moyo wake, aweza kutamani na hatimaye hata kutenda mambo ambayo hatima yake ni kuanguka kwenye utumwa wa dhambi daima.

Mshana akifafanua fundisho la Paulo anasema; Paulo anafundisha akiwasihi wagalatia pale alipoandika waraka wake kwao, kwamba watunze uhuru wao walioupata kwa njia ya kifo cha Kristo msalabani. Tuulinde uhuru wetu ili tuwe huru daima (Gal. 5: 1 – 18). Paulo anatetea kwa nguvu zake zote fundisho la imani na uhuru wa Kikristo (Christian liberty) kwa kusema, “kwa hiyo simameni imara katika uungwana huo”. Hapa Paulo anawataka watu wa kanisa la Galatia wasimame imara na kuyashika mafundisho waliyofundishwa, waimarike katika imani na kuwa hodari huku wakitenda mambo yote katika upendo. Ukiwa mtu wa matendo mema yanayoongozwa na imani, utakuwa mwaminifu, shujaa na imara. Si rahisi shetani kuchezea maisha yako. Paulo anatoa wito kwao wasilale bali wakeshe! Anajua shetani anachukia fundisho la neema, uhuru, faraja na uzima. Shetani anapiga vita fundisho la wokovu ili watu wa Mungu wachoke njiani, wakate tama na kukosa uhuru wa maisha ya wokovu. Uhuru ambao Paulo ameupata katika mafundisho ya Yesu Kristo ni uhuru ambao hata shetani anauchukia! Ni uhuru ule ambao umeletwa na Kristo Mwokozi wetu kwa vile hatuwezi kujikomboa wenyewe. Ni uhuru utokao kwa Kristo ili tusiwe watumwa wa shetani. Yesu Kristo ndiye aliyekuja ili kutuweka huru, huru mbali na dhambi, huru mbali na mauti, huru mbali na utumwa, huru mbali na sheria, huru mbali na hasira na ghadhabu ya Mungu. Huu kweli ni uhuru wa ajabu tusioweza kuueleza kwa maneno wala kuuwaza itoshavyo. Kila amwaminiye Kristo (Luther) anao uhuru huo (Galatians, pg. 444).

Mwanadamu anaweza kuishi maisha ya kuvitoa viungo vyake kutumika katika uchafu na uasi. Hapa pia ni kwenda kinyume na mpango wa Mungu. Hivyo kuna utumwa wa aina mbili. Kwanza kuna utumwa wa dhambi na pili kuna utumwa wa haki. Utumwa wa dhambi ni hali nzima ya mwanadamu kuishi katika maisha ya utumwa, maisha ya dhambi ya kuendeshwa kwa kila kitu na shetani. Amejaa tama za kidunia na kufuata maisha ya giza. Mara nyingi ni mtu anayependa kufuata hisia zake mwenyewe na kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Utumwa wa haki ni hali ya mwanadamu kuwa chini ya mamlaka ya Mungu kwa kutii wokovu ulioletwa na Yesu Kristo na kuwekwa huru mbali na dhambi na kuwa mtumwa wa haki.

Ni heri kuwa mtumwa wa Mungu ambaye ndiye kweli inayotupa uhuru, kuliko kuwa mtumwa wa shetani ambaye anatufanya watenda dhambi na mwisho wake ni mauti ya kiroho. … wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (Rum. 3: 23). Utumwa wa dhambi unaletwa na mambo yote yanayosababishwa na tamaa za kimwili. (Gal. 5: 19-21). Mkristo hapa hana uhuru wa kiroho kama mfuasi wa Kristo. Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi, kwa kuwa anamtii shetani mleta mauti kwa sababu ya dhambi.

Hebu fikiri mfano wa baba anayekunywa pombe sana na kuchelewa kurudi nyumbani. Anarudi usiku sana, kisha anampiga mke wake na watoto na hata kuwatukana sana. Pia anawafukuza nje ya nyumba usiku huo wanaenda kulala kwa jirani. Kama vile haitoshi, huibomoa nyumba yake kwa kuvunja baadhi ya milango kwa hasira. Asubuhi anaamka akiwa amechoka sana na hata kushangaa sana, na anaanza kutengeneza kwanza milango ya nyumba yake kwa aibu! Anaanza hata kufikiri jinsi atakavyoweza kumtafuta mke wake na watoto huko walikolala asikokujua. Hajui kama watoto walikula au la, yeye mwenyewe hakumbuki kama alikula au la, lakini amechoka sana na ana njaa sana. Hata hivyo la kushangaza ni kwamba ataendelea kurudia kunywa pombe kila siku inayotoka kwa Mungu na hajifunzi kitu. Huyu sio mateka wa shetani ingawa inawezekana hajijui kama yeye ni mtumwa wa shetani? Laiti angeachana na ulevi akakaa na watoto wake wapendwa wanaompenda na mke wake pia, wakajenga familia yenye upendo na ushirikiano!! Mungu alijua kuwa endapo mwanadamu ataendelea kuishi kwenye maisha ya dhambi, ataendelea kupata hasara na mateso mengi sana akiwa bado anaishi hapa duniani.

Dhambi ni uasi, unawahusisha na wasiohusika – ni kwa sababu ya udhaifu wa kimwili, viungo vinatumika kufanya uchafu na kuleta uasi, hivyo kumkosea Mungu. Hali hii imemfanya mwanadamu kuwa mtumwa. Mwanadamu anatakiwa kufanya mambo muhimu sana ya kimapinduzi katika maisha ya kila siku. Tunafundishwa kila mara kwamba neno la Mungu ni taa na mwanga katika njia zetu za kila siku.Yesu anaonyesha faida na umuhimu wa kukaa katika neno la Mungu. Kukaa katika neno la Mungu kunamsaidia mwanadamu kufahamu siri nyingi na muhimu zilizopo katika uwepo wa Mungu. Ni kufahamu kweli, kwa kufahamu kweli ndipo tunapata kuwekwa huru. (Rum. 6: 18, 22). Kuwekwa huru ni kufanywa upya na kutengwa na dhambi, yaani kutakaswa na hatimaye uzima wa milele ambao ndio tumaini la kila mmoja wetu.

Bila Yesu Kristo hatuwezi kuondoka katika utumwa wa shetani. Hatutaweza kuwekwa huru na kuwa wakristo walio huru kweli kweli, tutashindwa. Baada ya kuupokea upendo wa Mungu na hatua aliyochukua ya kushuka kwa njia ya Yesu Kristo kuteseka na kufa kwa kutupenda upeo, ndipo sasa tunapaswa kuupokea kwa kukubali kifo cha msalaba na kuishi kwa kufuata neno la Mungu. Hapa lazima tuongozwe na Roho wa Mungu kutenda vyema. Matendo ya roho ndiyo yaletayo uhuru wa mkristo – hatakabiliwa na sheria, yaani viungo vyetu vikitumika kwa haki, tunatakaswa. Tukitakaswa, tunawekwa huru mbali na sheria au mauti au dhambi na kufanywa watumwa wa Mungu. Kuwa mtumwa wa Mungu ni kuishi katika utaratibu wa Mungu na kufuata mapenzi yake. Na mwisho wa maisha haya ni kuurithi uzima wa milele. Ni tofauti sana na kuwa mtumwa wa shetani ambaye anakuendesha kwa kutumia vishawishi vya aina mbalimbali na mwisho wake ni mauti ya jehanamu. Katika maisha huwezi kukaa pande mbili, ni budi tuwe upande mmoja. Ni upande gani utachagua? Mimi nakushawishi uchague kukaa na Mungu wa kweli huyu aliyekukomboa kutoka katika mikono ya ibilisi kwa njia ya kifo cha mwana wake mpendwa Yesu Kristo pale msalabani. Tukiwa watumwa wa Mungu waliotakaswa, tunakuwa na hazina yenye faida kubwa mbinguni ambayo mwisho wake ni uzima wa milele.

Tukitii kwa mioyo yetu tutakuwa huru na kuepuka sheria/hukumu. Inawezekana umemtumikia shetani muda wa kutosha, na unaona mwenyewe kuwa hujafaidi chochote, umekosana na ndugu zako au na familia yako, kwa sababu ya maovu unayofanya kila siku, hujui hata mahali kanisa lilipo, ukimwona mchungaji unajisikia vibaya kwani dhamiri yako inakushitaki, usiku unaweza kuota hata mambo mabaya uliyofanya mchana uliopita! Wakati mwingine unakosa raha yako ya kawaida na amani! Hebu jiulize ni lini utajisikia vizuri? Ni lini utakuwa na amani? Ni lini utakuwa huru? Sasa uje kwa Yesu ili uwe huru. Kukaa na Yesu kila dakika ya maisha kunatusaidia kuepuka tama za mwili na matendo mengine mabaya yasiyompendeza Mungu. Basi mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Karibu kwa Yesu maisha kamili yenye uhuru kamili.

Mchg. John Anderson Moshi,
Chuo cha Theolojia na Uinjilisti Mwika,
Moshi – Tanzania.
johnmoshi@yahoo.com
mwika@elct.org

 

 


(top)