Göttinger Predigten im Internet
ed. by U. Nembach, J. Neukirch, C. Dinkel, I. Karle

UTATU 16, OKTOBA 1, 2006
MAHUBIRI KUTOKA MATHAYO 18:1-19
Elia M. Mande
(->current sermons )


Ndugu mpendwa, katika somo hili Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, analeta kwetu ujumbe muhimu kuhusu unyenyekevu, makosa kwa ujumla, makosa yetu tukijikosesha sisi wenyewe, tukiwakosea na kuwakosesha watu wengine na zaidi ya hayo yote Bwana daima anamtafuta kila mmoja wetu aingie katika zizi lake.

ALIYE MKUBWA KATIKA UFALME WA MBINGUNI

Mpendwa, katika somo hili tunaona wanafunzi wanamwendea Bwana Yesu kwa swali likihusu ni nani aliye mkubwa katika Ufalme wa mbinguni. Katika ulimwengu huu watu wanatafuta mno ukuu. Iwe ni katika Taifa ama Mkoa ama Wilaya na hata katika Kijiji, Wengi huwa na tamaa ya ukuu. Wengi hutamani kuwa na cheo fulani na mamlaka. Hili lipo pia katika Kanisa la Kristo.

Hawa wanafunzi wa Bwana Yesu wanauliza swali kwmba huko mbinguni ni nani aliye mkubwa! Walimwuliza Kristo Yesu, “Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni?” Hakika yawezekana si katika kutaka kufahamu tu, lakini zaidi sana hawa wanafunzi walitamani wapate ukuu huko katika ufalme wa mbinguni. Ona tamaa ya ukuu! Tamaa ya cheo na madaraka. Tukitafakari kwa kina tunaona kuwa wanachotaka kufahamu si tu ni watu wa tabia ama sifa gani watakaokuwa wakubwa katika ufalme wa mbinguni. Wanataka kufahamu hao watakuwa ni nani kwa majina hasa. Wao wakiwa wanafunzi wake Kristo Yesu tena wakiwa mitume na watumishi wake tayari ilionekana roho ya kujiinua watakapoingia katika ufalme wa mbinguni. Hiyo ni roho ya kujiinua na kutafuta ukuu. Kutafuta ukuu katika ufalme wa mbinguni.

Ndugu mpendwa, hapa tunaona Bwana Yesu anawapa fundisho wanafunzi wake. Anawapa fundisho la msingi na muhimu kuhusu unyenyekevu. Hakuna mfano ulio wa hali ya juu zaidi kuhusu unyenyekevu tunaoweza kuupata zaidi ya Kristo Yesu mwenyewe. Tazama, alinyenyekea akaacha utukufu wake mbinguni, akazaliwa kama mwanadamu tena katika hali ya umaskini. Naye alinyenyekea hata mauti ya msalaba! Lakini hawa wanafunzi wanauliza, “Nani aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni atakayetawala pamoja naye?” Wao wanadhani wote wale walio na nafasi katika ufalme wa mbinguni ni wakubwa. Waliowakuu kweli ni wale walio wanyenyekevu na watenda mema. Tena, tazama, wanafikiri kwamba kuna ngazi ama madaraja ya ukuu katika ufalme wa Mungu. Wanafikiri labda kuna Mawaziri Wakuu. Tamaa ya ukuu na cheo na madaraka.

Ona, kuna mataifa hapa duniani hivi sasa hawana amani na utulivu na utengemano kwa sababu ya watu wachache wanaotaka kuwa wakubwa. Hao wanautafuta ukuu kwa njia mbalimbali, kama vile, kujinyakulia madaraka, kuondoa uhai wa wengine wanaowaona ni tishio kwa nafasi zao na hata kuongoza vita vya msituni na mapambano ya aina mbalimbali. Ndiyo! Si kwa mataifa tu bali hata katika makanisa yetu. Ona wale wana wa Zebedayo, Yakobo na Yohana, walivyoutafuta ukuu katika ufalme wa mbinguni. Walimwendea Bwana Yesu na kusema, :”Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.” Marko 10:37. Wanatafuta ukuu katika ufalme wa mbinguni wangali bado wapo hapa duniani.

Kuna baadhi ya makanisa yanakosa upendo, amani na umoja kwa sababu ya wale wachache wanaotafuta na hata kung’ang’ania katika ngazi mbalimbali za ukuu kanisani.

Ndugu mpendwa, kuna mfano hai mmoja wa ajabu lakini ni wa kweli na ulitokea katika kanisa moja kwa mmoja wa viongozi wa kanisa hilo. Huyo aliutafuta ukuu kwa njia ya giza kabisa. Aliutafuta ukuu kanisani kwa njia ya kwenda kwa mganga wa kienyeji na kupewa maelekezo na masharti ya kutoa kafara ili kuchaguliwa kuwa mkuu katika kanisa hilo. Aliambiwa na mganga kumtoa kafara mtoto wake wa kumzaa kwa kutoa uhai naye angeshinda katika uchaguzi wa kumchagua mkuu wa kanisa hilo. Kweli alitekeleza hilo. Naye alichaguliwa. Lakini jambo la ajabu lililotokea ni wakati wake wa kusimikwa kazini. Aliposimama mbele madhabahuni yule mtoto wake aliyemwua yeye alimwona kana kwamba anasimama mbele yake. Hivyo alianguka na kuzimia pale madhabahuni. Baadaye alipopata fahamu na kusimama tena madhabahuni kwa kusimikwa alimwona tena mtoto wake anasimama mbele yake. Naye alianguka tena na kuzimia. Onyo la aina yake kwa wale wote wanaotafuta ukuu hata kanisani kwa njia za giza.

Ni nani basi atakayekuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni? Katika Neno la Mungu tunasoma kwamba Bwana Yesu, “Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” Mathayo 18:2-3. Unyenyekevu ni somo muhimu mno kujifunza kwa njia ya mfano huu anaoutoa Bwana Yesu kwa wanafunzi wake na kwa wale wote walio wafuasi wake hata hivi leo katika karne hii ya 21. Tunapomtazama mtoto mdogo, tukumbushwe jinsi Kristo alivyomtumia mtoto kutufundisha kuhusu unyenyekevu na kuingia katika ufalme wake wa mbinguni. Alimweka mtoto katikati yao, sio kwamba wacheze na huyu mtoto bali wapate kujifunza kutoka huyu mtoto.

UWE NA UNYENYEKEVU NAWE UTAINGIA KATIKA UFLAME WA MBINGUNI

Ndugu mpendwa, hapa tunaona wazi umuhimu wa unyenyekevu katika maisha haya na katika maisha yale yajayo katika ufalme wa Mungu. Kristo Yesu anakaza akisema, “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. “ Hapa tunaona na kujifunza, kwanza, ni lazima tuongoke. Ni lazima tugeuke kwa upya na kumrudia Bwana Mungu wetu na Muumba wetu. Tuongoke katika mawazo yetu, katika maneno yetu na katika matendo yetu na tabia zetu. Ndiyo, yatupasa kutubu sasa. Pili, tunaona na kujifunza kuwa ni lazima tuwe kama watoto wadogo. Sisi sote tunafahamu jinsi watoto walivyo, wamejaa furaha, upendo na ni wepesi kusikia na kutumwa na kusamehe na mengine mengi ya jinsi hii. Nasi vivyo hivyo, tuwe kama watoto wadogo. Neema ya Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wetu inayookoa, hutufanya sisi kuwa kama watoto wadogo. Tukiwa kama watoto hatutajihangaisha mno na maisha yetu bali zaidi sana tutamwachia Baba yetu wa mbinguni atutunze sawasawa na mapenzi yake. “Msisumbuke, basi, mkisema, tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? … kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.” Mathayo 6:31-32.

Ndugu mpendwa, yatupasa kuwa wanyenyekevu kama watoto wadogo. Tazama, umri wa utoto ni umri wa kujifunza. Nasi kwa ujumbe huu tujifunze unyenyekevu, tena tufunuliwe na kuona na kufahamu hatari kuu ya kujiinua. Ona! Kiburi na kujiinua kuliwafanya malaika waliofanya dhambi watoke mbinguni. Ndivyo itakavyokuwa pia kwa wale wote wanaolisikia Neno la Mungu bila ya kulishika na kutenda kama Neno linavyoagiza. Na ndugu mpendwa iwapo dhambi hiyo inatawala mioyo yetu na maisha yetu na hakika tusipotubu hivi sasa kama anavyoonya Kristo Yesu mwenywe katika ujumbe huu hatutaingia katika ufalme wake wa mbinguni. Mahubiri ya kwanza ya Bwana Yesu yalikuwa, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni, na kuiamini Injilia.” Marko 1:15.

VIKWAZO

Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo anaonya pia katika somo hili juu ya vikwazo. Mambo ya kukwaza na kukwazana ni mengi katika maisha yetu ya siku kwa siku. Mambo ya kukosesha pia ni mengi. Biblia inasema, “Basi mkono wako au mguu wako ukikusesha, ukate! Ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ukalitupe mbali nawe, ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho mwili, na kutupwa katika jehanam ya moto.” Mathayo 18:8-9.

Majaribu mengi ya kutuangusha dhambini yanatoka ndani mwetu. Basi, inatupasa tuwe macho daima. Angalieni sana jinsi mnavyoenenda, angalieni sana jinsi mnavyoishi. Tuwe na hekima, zaidi, tusimame imara katika Imani iliyo hai katika Yesu Kristo, hakika tutaishinda na hatimaye kuuingia na kuurithi uzima wa milele katika ufalme wake Kristo Bwana.

MFANO WA KONDOO ALIYEPOTEA

Ndugu mpendwa, Neno la Mungu linatoa wito maalum kwa watu wote ambao wako nje ya zizi la Bwana, kuwa ni kama kondoo aliyepotea. Usiku na mchana Bwana Mungu anawatafuta hao wote ili nao waje zizini kwa Mchungaji Mkuu wa Kondoo, Yesu Kristo. Hata mmojawao anapopokelewa kundini kunakuwa na furaha na mashangilio hapa duniani na mbinguni pia. Malaika mbinguni wanamshangilia Bwana kwa nyimbo za sifa.

Mpendwa, ujumbe huu unakuja kwako hivi leo kuleta wito huo mkuu wa kutubu na kumwamini Yesu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu, nawe kwa hakika, utapata raha nafsini mwako. Nawe utapata amani ya kweli na furaha ya kweli katika Kristo. Utapata wokovu, uzima wa milele kuanzia hapa hapa duniani hadi utakapoimba: “HALELUYA!” milele na milele katika ufalme wa mbinguni.

Ninakuombea neema na baraka za Mugnu katika maisha yako ya kiroho na kimwili.

“Na amani ya Mungu ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” (Wafilipi 4:7), Amin.

Mch. Elia M. Mande,
Chuo cha Biblia na Theologia Mwika,
S.L.P. 3050,
Moshi - Tanzania
E-mail: mwika@elct.org

 

 


(top)